EXCLUSIVE--SAMWEL SITTA AZIDI KUIBIA NCHI,ATUMIA UBABE WAKE KUFUJA MALI ZA UMMA SOMA HAPO KUPATA ZAIDI
Na Pendo Omary
KITENDO cha mbunge wa Urambo (CCM), Samwel Sitta, kung’ang’ania nyumba mbili za serikali zilizotengwa kwa ajili ya makazi rasmi ya spika wa Bunge, kinaingiza serikali hasara ya mamilioni ya shingi, imefahamika.
Nyaraka ambazo Chanzo hicho imeziona zinaonesha ofisi ya bunge inagharamia kila mwezi, malazi ya spika wake wa sasa Anne Makinda; pamoja na gharama nyingine zikiwamo ukarabati, mapazia, mazulia, viyoyozi na vifaa vya kufanyia usafi.
Nyumba mbili ambazo zimekodishwa na serikali na kutengwa kwa makazi rasmi ya spika na ambazo Sitta anazing’ang’ania, ni ile ya jijini Dar es Salaam na nyingine iko mjini Dodoma.
Jijini Dar es Salaam, nyumba hiyo ipo Barabara ya Buzwagi, Masaki. Kila mwezi serikali inalipa kiasi cha Dola 8,000 (zaidi ya Sh. 12 milioni) kwa nyumba hiyo. Mjini Dodoma, nyumba ambayo Sitta amegoma kuhama, ipo katika eneo la Area C. Haikufahamika inalipiwa kiasi gani.
Kwa mujibu wa nyaraka hizo, ofisi ya Bunge inapaswa kulipa kiasi cha Sh. 18.10 milioni kwa ajili ya kufanyia marekebisho nyumba binafsi ya Makinda ambayo iko maeneo ya Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Aidha, serikali inapaswa kulipa kiasi kingine cha Sh. 6,085,000 kwa ajili ya kilichoitwa, “ufungaji wa mapazia na mazulia katika makazi ya spika wake.”
Kiasi kingine cha Sh. 12.6 milioni kimelipwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufanyia usafi makazi ya Makinda yaliyoko Dodoma.
Mamilioni hayo ya shilingi yamelipwa kwa makampuni ya Lerai Laundry & General Supplies na Constantine M. Kubena.
Kwa mujibu wa mchanganuo wa madeni inayodaiwa ofisi ya Bunge yanayofikia zaidi ya Sh. 5 bilioni ambao umepelekwa wizara ya fedha, kiasi cha Sh. 36 milioni, zimetumika kwa kazi hizo.
Chanzo hicho kimeshindwa kuelewa iwapo vifaa hivyo vilivyonunuliwa na serikali; ambavyo vinatumika katika makazi rasmi ya spika, vitarejeshwa serikalini wakati spika huyo atakapoondoka; au vitakuwa mali yake.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo, hakupatikana kwa kuwa amedaiwa yuko nje ya nchi kikazi.
Simu yake ilipokewa mara mbili, lakini hakukuwa na mtu aliyeongea. Ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms) uliotumwa ili kuomba ufafanuzi, haukujibiwa hadi Chanzo hicho kinakwenda mitamboni.
Naye Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, aligoma kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa hajabahatika kuona nyaraka ambazo Chanzo hicho inatumia.
“Siwezi kukueleza chochote kuhusu uhalali au deni hilo. Nyaraka unayosema sijaiona; kwa hivyo si rahisi mimi kuzungumzia hilo,” alisema.
Nyaraka ambazo mtoa habari amezieleza, zimetumwa hadi kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo MwanaHALISI Forum.
Kupitia ukaguzi kwenye nyaraka uliofanywa na Chanzo hicho, hakuna kilichoonekana kusomeka kuhusu kampuni ya Constantine M. Kubena na kwa hivyo imekuwa vigumu kuthibitisha taarifa zake kama ni kampuni iliyosajiliwa.
Kwa upande mwingine, ukaguzi huo umeshindwa kupata taarifa za iitwayo Lerai Laundry & General Supplies; bali kulikutwa Lerai Laundry and General Cleaner, yenye anuani ya posta 2672, Dodoma.
Chanzo hicho kilishindwa kupata mhusika wa Lerai Laundry and General Cleaner kwani namba za simu ya mkononi zilizowekwa kwenye anuani hiyo ya mkoani Dodoma – 0754 443072 na 0718 676722 – hazikuwa na majibu kwa muda mrefu zilipopigwa juzi.
Kampuni hiyo imeoneshwa kuwa inashughulikia usambazaji wa vifaa vya kusafishia majengo.
Taarifa hizi zinakuja wakati tayari serikali imegharimia matengenezo ya nyumba ya Makinda iliyoko Kijitonyama, Dar es Salaam ambayo ujenzi wake ulikumbana na lawama kali za wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo.
Makinda analaumiwa na majirani zake kwa kusababishia usumbufu kwa kuziba njia inayopita katika eneo hilo kwenda maeneo ya vitongoji vya Sinza.
Sheria ya mafao ya viongozi wastaafu wa siasa haisemi mahali popote spika mstaafu anapewa nyumba na serikali. Sheria inatamka spika mstaafu kupewa gari moja ambalo atalihudumia mwenyewe, na dereva.
Gari hilo litahudumiwa na bunge kwa matengenezo; na atapewa lita 70 za mafuta kwa ajili ya gari hilo.
Lakini Sitta ni mbunge wa Bunge la Muungano. Kwa nafasi hii, kila mwezi analipwa na serikali lita 1,000 za mafuta kwa bei ya Sh. 2,500 kwa lita.
Serikali inamlipa Sitta posho za kujikimu kwa kila anapokuwa katika mikutano ya Bunge au kamati za bunge; hili linafanywa kwa mawaziri wote na naibu wao wanapokuwa katika vikao vya bunge.
Mawaziri na naibu wao wanapewa gari na serikali, wanapewa nyumba; na kwa wale wanaoishi katika nyumba zao, hulipwa na serikali fedha kama fidia ya gharama za nyumba. Hata hivyo, nyumba hizo hazina hadhi ya makazi ya spika.
Taarifa zilizowahi kuchapishwa katika vyombo vya habari miaka mitatu iliyopita zinasema, tangu Sitta ang’olewe katika kiti cha spika mwaka 2010, ameng’ang’ania makazi ya spika, kutokana na kile kinachoitwa, “makubaliano yake na Rais Jakaya Kikwete.”
Mbali na kung’ang’ania makazi ya spika, waziri huyo wa Afrika Mashariki, ameng’ang’ania walinzi wawili waliokuwa wanamlinda.
Makubaliano kati ya mkuu huyo wa nchi na Sitta ambaye anatajwa kuwa alikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi katika kundi la wanamtandao waliomuingiza Kikwete madarakani, yalitokana na hatua ya Kamati Kuu (CC) ya CCM, kumeungua Sitta katika kinyang’anyiro cha spika.
Katika hatua nyingine, ofisi ya Bunge imetumia kiasi cha Sh. 4.2 milioni kwa ajili ya kununulia pipi; Sh. 10.6 milioni kwa ajili ya maji, juisi iliyotumiwa na viongozi, wakuu wa idara na vitengo; na zahanati ya bunge.
Fedha hizo zimelipwa kwa kampuni ya Pongai Enterprises; Kilya Enteprises na Robert Ngwigulu.
Chanzo ni GAZETI LA MAWIO
Hakuna maoni
Chapisha Maoni