Zinazobamba

CAG AIPA HATI CHAFU CHAMA CHA CCM ,NA AIBUA MADUDU YA MENGI, SOMA HAPA KUJUA ZAIDI

1
Na Betty Kangonga 
   SIKU chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kukiri kupokea hati ya mashaka kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kumtaka aweke hadharani hesabu za vyama vingine, hatimaye imebainika kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimepata hati kama hiyo.
Hatua hiyo ilibainika jana wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo kwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa na CAG.
Msaidizi wa ofisi ya CAG, Benja Majura alivitaja vyama vilivyopata hati zenye mashaka baada ya hesabu zake kuwa na mapungufu ya kiuhasibu kuwa ni CCM, CHADEMA, CUF, TLP na NCCR-Mageuzi.
Ukaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa sheria namba 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, iliyofanyiwa marekebisho na sheria namba 7 ya mwaka 2009, unampa CAG mamlaka ya kukagua hesabu za vyama vya siasa.
Katika mwaka wa fedha 2012/13 Msajili wa Vyama vya siasa alitoa ruzuku ya sh.16.8 bilioni kwa vyama nane vya siasa ambavyo ni CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP, APPT-Maendeleo na DP.
Vyama hivyo ni kati ya 12 vilivyowasilisha hesabu zake kwa CAG, ambapo vipo pia ambavyo vimepata hati mbaya na chafu.
Majura alivitaja vyama vilivyopata hati chafu kwa kuwa hesabu zake hazikueleweka kuwa ni NRA, UMD, APPT-Maendeleo, NLD, ADC, SAU na Chaumma.
Alivitaja vyama ambavyo havijawasilisha hesabu zake na kufanyiwa ukaguzi kuwa ni pamoja na Tadea, UPDP, UDP, Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema kuwa ukaguzi huo umekumbana na changamato mbalimbali ikiwemo kukosa muongozo wa muundo wa kuandaa taarifa za kifedha kwa vyama hivyo, kutoa karatasi moja ya mahesabu, vyama kutokuwa na ofisi, ukosefu wa vitendea kazi.
Naye Jaji Francis Mutungi, alisema kuwa kati ya vyama hivyo vilivyokaguliwa UMD, NLD, APPT-Maendeleo, ADC, CCM na CUF vimewasilisha ukaguzi huo katika ofisi yake.
Alisema kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na TLP havijawasilisha ukaguzi huo katika ofisi yake licha ya kukaguliwa.


Jaji Mutungi alivitaka vyama ambavyo havijawasilisha taarifa hizo katika ofisi yake kuhakikisha wanawasilisha taarifa hiyo kabla ya Oktoba 31 mwaka huu.

Hakuna maoni