Zinazobamba

WAZIRI ULEGA AMEIAGIZA TBA KUHAKIKISHA NYUMBA ZA TEMEKE KOTA ZINAWANUFAISHA VIJANA WANAOINGIA KWENYE UTUMISHI WA UMMA.


Waziri Ulega akichanganya udongo wa saruji(Cement)katika Jendo la mradi wa nyumba 144 wa  Temeke Kota unaotekelezwa na TBA Wilayani Temeke

*Amesisitiza mchakato wa uwazi utumike kuwapata vijana wenye vigezo vya kupata nyumba hizo.

*Azuia kutumika madalali kwenye nyumba hizo.

Na Mussa Augustine.

Waziri wa Ujenzi Mh. Abdalah Ulega ameagiza Wakala wa Majengo Nchini (TBA) kuhakikisha nyumba za mradi wa Temeke Kota zinawanufaisha vijana wanaoingia kwenye utumishi wa umma kama ilivyoelekezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia ameagiza TBA kushirikiana na sekta binafsi ili kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 inayoelekeza kufanikisha upatikani wa makazi bora yenye bei nafuu kwa wananchi, hususan vijana wanaojitafuta kimaisha.

Waziri Ulega ametoa maagizo hayo leo Mei 3,2026, wakati alipotembelea mradi wa nyumba 144 unaojengwa na TBA wilayani Temeke,na kuongeza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha watumishi wa Serikali wanaoajiriwa wanapata nyumba za bei nafuu kwa ajili ya kuanzia maisha.

"Nimekuja kuona mradi huu wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambazo zipo hapa Temeke Kota. Napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TBA na timu yake. Nimeona mradi ni mzuri. 

Huu mradi una jumla ya nyumba 144. Kati ya nyumba hizi, nyumba 72 ni za chumba kimoja, sebule na choo, lakini nyumba nyingine 72 ni zile zenye masta, chumba kidogo na sebule kubwa kwa ajili ya wale wenye familia ndogo," amesema.
Waziri Ulega akikagua Jendo la mradi wa nyumba 144 wa Temeke Kota unaotekelezwa na TBA Wiyani Temeke

Na kuongeza kwamba, "Nimekuja kukagua kwa sababu ni kazi aliyoelekeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kututuma sisi kuhakikisha tunafanya kazi ya kutafuta suluhu inayohusu nyumba za bei nafuu kwa wananchi, hususan kundi la vijana."

Aidha, ameendelea kusema kuwa nyumba zilizojengwa Temeke Kota zitakuwa za vijana wanaoingia kwenye utumishi wa umma, ambapo mpango mpana wa Dira ya Rais Dkt. Samia ni kujenga nyumba za jumla kwa ajili ya vijana wote ambao ni watumishi wa umma na wale ambao si watumishi wa umma.

"Naielekeza TBA kutafuta wabia kutoka sekta binafsi. Rais Dkt. Samia anatusisitiza kwenye miradi yote ya majengo, barabara na vivuko tushirikiane na sekta binafsi.Sisi Serikali peke yetu hatuwezi kufanya yote hayo," amesema.

Na kuongeza kuwa, "TBA wamenieleza kuwa pango la nyumba hizi litakuwa na bei kati ya laki mbili (200,000) hadi laki tatu na elfu hamsini (350,000).Nimetazama bei ya soko,mimi binafsi kama Waziri nimeridhika kuwa hiyo bei kwa hapa Temeke ni bei muafaka kabisa," amesema.
Jengo la mradi wa nyumba 144 wa  Temeke Kota unaotekelezwa na TBA Wilayani Temeke.

Aidha, amesema kuwa vijana wengi wanahangaika kupata makazi bora na ya bei nafuu, hivyo ameitaka TBA kuacha kutumia madalali kwenye nyumba hizo, na mchakato uwe wa uwazi wa kupata vijana wenye sifa ya kupanga nyumba hizo, ikiwemo kutangaza vigezo hivyo kwenye vyombo vya habari, ikiwemo magazeti na mitandao ya kijamii.

"Tangazeni vigezo hadharani, maana watakaoomba ni wengi na hawawezi kupata wote, lakini hata wale vijana watumishi wanaojitafuta watakaokosa wataridhika kwa sababu mchakato utakuwa wa uwazi. Msifanye ujanja wa kuwapatia vijana ambao hawana vigezo," amesisitiza Waziri huyo.
Jendo la mradi wa nyumba 144 wa  Temeke Kota unaotekelezwa na TBA Wilayani Temeke

Aidha, amesema mpango wa Serikali ni kujenga nyumba nyingi zaidi kulingana na malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo 2050,nyumba za makazi ya bei nafuu (Affordable Housing),ambapo TBA itahakikisha inatekeleza miradi hiyo katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha,Mbeya na Dodoma.

Kwa upande wake,Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke Uzairu Abdul Athuman ameishukuru Serikali na TBA kwa kujenga mradi huo wa Temeke Kota, kwani utasaidia vijana wanaoingia kwenye utumishi katika wilaya hiyo, huku akisisitiza kuwa watahakikisha wanasimamia maelekezo yote ya Serikali.


No comments