HALI YA ULINZI NA USALAMA SIKUKUU YA EID IMEIMARISHWA:SACP MULIRO
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewahakikishia wananchi kuwepo kwa ulinzi wa kutosha wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Eid el-Fitri, huku likieleza kuwa hali ya usalama jijini humo inaendelea kuwa nzuri.
Akitoa taarifa kwa umma Machi 20, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP. Jumanne Muliro amesema wananchi wameendelea kushirikiana vyema na jeshi hilo katika juhudi za kuzuia vitendo vya uhalifu, hali inayochangia utulivu wa jiji.
Katika hatua nyingine,ameeleza kuwa Jeshi hilo la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili akiwemo mwanamke aitwaye Rehema Maulidi (42), mkazi wa Kigamboni, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Athumani Nyanza, ambaye mwili wake ulipatikana umefukiwa karibu na makazi yake katika eneo la Zingiziwa, Ilala. Uchunguzi unaendelea huku taratibu za kisheria zikikamilishwa.
Aidha,jeshi hilo limebainisha mafanikio yaliyopatikana mahakamani ambapo watuhumiwa kadhaa wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali jela kati ya Februari 25 na Machi 18, 2026.
Miongoni mwa waliotiwa hatiani ni Joel Israel na Athuman Saidi, wote wakazi wa Dar es Salaam, waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wengine ni pamoja na Majid Kassim aliyepata kifungo cha miaka 20 kwa kosa la shambulio la aibu, pamoja na Simon Lesirwa na Omar Yasin waliopata vifungo vya miaka 30 jela kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ubakaji mtawalia.
Hata hivyo Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola,hasa katika kipindi hiki cha sikukuu,ili kuhakikisha usalama unaendelea kudumishwa.
“Tunawahakikishia wananchi wote wa Dar es Salaam kuwa ulinzi umeimarishwa,hivyo waadhimishe sikukuu ya Eid kwa amani na utulivu,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Jeshi hilo pia limewatakia wananchi wote sikukuu njema ya Eid el-Fitri.

No comments
Post a Comment