CUF BADO NA MSIMAMO WAKE WA KUUNDWA SERIKALI YA MPITO MWAKA HUU 2026
```THE CIVIC UNITED FRONT(CUF-Chama Cha Wananchi)
MSIMAMO WA CUF JUU YA KUUNDA SERIKALI YA MPITO MWAKA HUU 2026 KAMA NJIA PEKEE YA KULITIBU TAIFA NA KUHAKIKISHA MUAFAKA NA MARIDHIANO YA KWELI:
CUF – Chama Cha Wananchi, kikizungumza kwa niaba ya wananchi wa Tanzania, kinatoa tamko rasmi la kisiasa kuhusu hitaji la Taifa kuingia katika mchakato wa Serikali ya Mpito ya Kitaifa.
Chama chetu kinatambua kuwa nchi imeingia katika mkwamo mkubwa wa kikatiba, kisiasa na kidemokrasia unaodhihirishwa na migogoro ya uchaguzi, kudhoofika kwa taasisi huru, na kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa mifumo ya dola.
CUF-Chama Cha Wananchi tunatambua wazi kwamba, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna utaratibu unaotambua au kuruhusu kuundwa kwa Serikali ya Mpito. Hivyo basi, kuanzishwa kwa Serikali ya Mpito ni lazima kutanguliwe na marekebisho ya Katiba iliyopo, ili kutoa uhalali wa kisheria wa muundo huo wa mpito.
Marekebisho hayo ya Katiba yataweka bayana:
* Msingi wa kikatiba wa Serikali ya Mpito
* Muda wake wa kuwepo
* Mamlaka na mipaka yake
* Mahusiano yake na mihimili mingine ya dola
MSIMAMO RASMI WA CUF
CUF inasisitiza kuwa Tanzania inahitaji suluhisho la kitaifa, si la kichama. Serikali ya Mpito inapendekezwa kama daraja la maridhiano, haki na mageuzi ya kweli, si mapinduzi.
Majukumu makuu ya Serikali ya Mpito, kama inavyoonekana na CUF, ni pamoja na:
Kulazimisha na kusimamia marekebisho ya Katiba na kisheria;
Kutekeleza marekebisho ya sheria kuhakikisha demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria;
Kurekebisha sheria za uchaguzi, vyama vya siasa na uendeshaji wa taasisi huru;
Kuweka masharti mapya ya kisheria kuhakikisha uhuru na uwajibikaji wa Tume ya Uchaguzi;na
Kuunda mazingira ya kisheria yanayolinda haki za kisiasa, kiraia na uhuru wa maoni.
MASHARTI MUHIMU KUHUSU SERIKALI YA MPITO:
Serikali ya Mpito lazima:
1. Iwe ya muda maalum na usiozidi makubaliano ya kitaifa
2. Ijumuishwe vyama vyote vya siasa na makundi ya kijamii
3. Viongozi wake wasitumie nafasi hizo kama daraja la kugombea madaraka baada ya mpito.
Ndugu wanahabari!
CUF inaamini Tanzania imefika mahali pa kuchagua kati ya kuendeleza mkwamo wa kisiasa au kufungua ukurasa mpya wa maridhiano na haki. Migogoro ya uchaguzi na kudhoofika kwa taasisi vimepunguza imani ya wananchi.
Ndiyo maana CUF inapendekeza kuanzishwa kwa Serikali ya Mpito ya Kitaifa yenye muda maalum, itakayoshughulikia Katiba Mpya, mageuzi ya uchaguzi na maandalizi ya uchaguzi huru na wa haki.
Hii si ajenda ya chama, bali ni ajenda ya Taifa.
HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!```
Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Januari Mosi, 2026```
No comments
Post a Comment