Zinazobamba

WAZIRI KAPINGA AIPA KONGOLE FCC KWA KUTOA HUDUMA NZURI KWA WATANZANIA


Na Mussa Augustine.

Waziri wa Viwanda na Biashara,Judith Kapinga ameipongeza Tume ya ushindani (FCC)kwa kazi kubwa na nzuri inayoifanya kuhakikisha inadhibiti bidhaa bandia na kumlinda mlaji.

Waziri Kapinga ametoa pongezi hizo mapema leo Novemba 24,2025 Jijini Dar es salaam wakati alipoitembelea tume hiyo kwa lengo la kuzungumza na Watendaji wa tume hiyo ikiwa ni kuimarisha misingi ya utekelezaji wa majukumu  ya tume pamoja Wizara yake kwa ujumla.

"Tume hii ya ushindani ni tume muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa letu,ndo Tume ambayo ina jukumu kubwa sana kwenye masuala ya udhibiti,lakini pia kwenye masuala ya kulinda walaji, udhibiti wa bidhaa feki,Elimu kwa umma, pamoja na masuala mengine ya kibiashara ikiwemo muunganiko wa makampuni makubwa ili kuhakikisha muunganiko huo unaendelea kua shindani lakini wenye manufaa na unaweka ustahimilivu wa biashara."amesema 

Nakuongeza kuwa" Leo tumefika hapa tumefanya kikao cha ndani kwa ajili ya kuimarishana katika utekelezaji wa shughuli zetu,Tume ya ushindani(FCC) imekua ikifanya majukumu yake vizuri sana,matokeo mengi ambayo yanaonekana kwenye jamii ni kwasababu ya kazi kubwa inayofanywa na Tume hii".

Aidha amesema kuwa ziara yake imelenga kuongeza misingi ambayo imewekwa kwa ajili ya kuongeza ubora na ufanisi,nakwamba Watanzania wanaitegemea Wizara ya Viwanda na biashara kupitia taasisi zake za udhibiti na uratibu ikiwemo FCC ambayo imekua ikiboresha namna nzuri ya utendaji kazi,ili kufikia mategemeo ya Watanzania ambao ndo walaji. 

"Vilevile tumeendelea kuhimizana kuhusiana na masuala ya udhibiti,namna bora yakufanya ili kudhibiti bidhaa feki,ambayo ndo mategemeo makubwa sana kwa Watanzania,kwasasa tupo katika ulimwengu wa tofauti sana,na Mazingira ya biashara yanatofautiana kutoka siku ya kwanza mpaka siku nyingine,
kwahiyo tumewekeana mikakati mizuri yakuhakikisha tunaboresha ufanisi lakini tunaongeza ubunifu kwa kuongeza mikakati ya kushirikiana na Sekta binafsi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yetu." amesema Waziri Kapinga ambaye ameambatana na Naibu Waziri Patrobas Katambi.

Nakusisitiza kwamba "Kwakweli kikao chetu cha leo kililenga  kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Tume yetu ya ushindani ambayo tayari inafanya kazi nzuri lakini yapo mambo ambayo tumekubaliana inabidi tuyaongeze kwa ajili ya kuboresha ufanisi zaidi."

Akizungumzia Mikakati ya Wizara ya Viwanda na biashara katika kuongeza mapato ya nje Waziri Kapinga amesema kuwa moja ya mikakati waliyonayo ni pamoja na  kuendelea kuongeza kongani za Viwanda kwasababu kupitia Viwanda kutaongeza mapato ya nje,kuongeza ajira pamoja na  mapato ya ndani. 

"Vilevile kuendelea kutekeleza sera zetu ambazo ni himilivu,tunazo sera ambazo ni kuu lakini pia tumekua tunakuja na sera mbalimbali kulingana na mabadiliko ya Mazingira ya biashara ambayo yanatokea mara kwa mara." Amesema 

Amesema kuwa Sekta ya Viwanda na biashara ni sekta ya uratibu,ambayo inashirikiana na sekta nyingine nyingi hivyo sekta hiyo imeendelea kuongeza uratibu ili kuhakikisha Mazingira yakufanya Biashara Tanzania yanapunguza urasimu,lakini pia yanaendelea kua rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara pamoja na Watanzania wa kawaida ambao kila siku wanatamani kufanya biashara. 
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Bi.Hadija Juma Ngasongwa amesema kwamba hali ya ufanyaji wa biashara Tanzania inakua siku hadi siku,lakini FCC ikiwa miongoni mwa taasisi ya kudhibiti na kuratibu,kwa sasa haifanyi sana udhibiti pekee lakini inafanya zaidi uratibu.

"Tunafanya zaidi uratibu kwa maana ya kwamba tunaingia kwenye ile falsafa ya mheshimiwa Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwamba vyombo hivi visaidie kuwezesha kutoa majibu na kutoa kero za Wananchi hasa katika ufanyaji wa biashara kupitia falsafa ya kukuza uwekezaji nchini." amesema Bi.Ngasongwa

Nakuongeza kuwa"Kwasasa uwekezaji umekua mkubwa sana,na sisi taasisi yetu ni moja ya taasisi ambayo tunapitia, na tunachambua miamala ya Muunganiko wa makampuni kwa lengo la kukuza mitaji,kuokoa ajira ambazo kwa baadhi ya kampuni au Viwanda ambazo zimeonekana zimeweza kuzorotisha.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo wa FCC amesema kwamba  ziara ya Waziri wa Viwanda na biashara Judith Kapinga na Naibu Waziri Patrobasi Katambi kutembelea tume hiyo imewapa motisha kubwa ya kuendelea kufanya kazi vizuri Kwa ajili ya kuendelea kuwahudumia Wafanyabiashara na wawekezaji kwa usawa.
"Kwa sisi ujiuo huu wa Waziri na falsafa hii ya kuweza kuwafikia Wananchi imetupa motisha na tumefarijika sana kwa maana kwamba katika taasisi 13 ambazo zipo chini ya Wizara ya Viwanda na biashara leo ameweza kututembelea,na ameweza kujifunza Majukumu yetu makubwa kwanza tunaimarisha ufanyaji wa biashara uendane na nguvu ya soko katika hatua ya kiushindani zaidi na sio kutumia hila wala mabavu bali kufuata misingi ya usawa."amesema.



No comments