Zinazobamba

WAUMINI WA BCIC MAJIMEUPE WATOA MSAADA HOSPITALI YA MAJI MATITU KUELEKEA MAADHIMISHO YA MIAKA 15.



Na Mussa Augustine.

Waumini wa Kanisa la BCIC Majimeupe  Kanda ya Dar es salaam wametoa zawadi ya vifaa mbalimbali ikiwemo viti,sabuni,taulo za kike,mifagio nakufanya usafi  katika hospitali ya Maji Matitu kwa ajili ya kuwasaidia wakina mama wajawazito wenye mahitaji mbalimbali.

Akizungumza leo Juni 8,2024 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Askofu Mkuu msaidizi wa BCIC Majimeupe kanda hiyo Askofu Michael Petter Imani amesema kuwa hatua hiyo inatokana na kuelekea maadhimisho ya miaka kumi na tano ya kanisa hilo inayotarajiwa kufanyika siku ya jumapili ya tarehe 9 Juni ,2024.

Askofu Imani ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanda ya Dar es salaamu na Pwani pamoja na Mchungaji kiongozi wa kanisa hilo, amesema kuwa BCIC Majimeupe limefanya mambo mengi yakujivunia ndani ya miaka kumi na tano ya uinjilishaji ikiwemo kubadilisha tabia ovu za baadhi ya watu nakuwafanya waachane na matendo mabaya kama vile ulevi,uasherati pamoja na wizi.

“BCIC Majimeupe kesho tunaadhimisha miaka kumi na tano tangu kuanzishwa kwa kanisa hili hapa mbagala majimatitu mwaka 2009,hivyo leo tumekuja hapa hospitalini ili kutoa mchango wetu mdogo wa vifaa mbalimbali ikiwemo sabuni,viti,taulo za kike na fedha kidogo ikiwa ni sehemu ya kuwakumbuka wagonjwa na kuwafariji “amesema Askofu Imani.

Nakuongeza kuwa”Kulikua na mambo mengi mabaya hapa maji matitu yakiwemo masuala ya ushirikina hadi watu walikua wanashindwa hata kujenga nyumba na barabara lakini tangu BCIC Majimeupe kuanzishwa hali imebadirika sana,kwa sasa tuna waumini takribani 2000 na wananchi wengi wanajitokeza kumpokea yesu kristo kuwa mwokozi wa maisha yao.

Aidha ametoa wito kwa waumini na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kusherehekea maadhimisho hayo ya miaka kumi na tano yatakayoanza mapema asubuhi nakutamatika jioni.

Kwa upande wake Mwenyekiti Bodi ya Afya wa Kituo cha Afya Maji Matitu Bi.Hadija Hassan Ndende amewashukuru waumini hao kwa kujitoa kwa kusaidia wakina mama wajawazito wenye mahitaji muhimu kwa kuwapatia msaada huo.

“Tunashukuru sana BCIC Majimeupe kwa kutuletea msaada huu ,sio mara ya kwanza kwenu kuja hapa,tunaomba muendelee na moyo wenu wa huruma na mungu awazidishie maradufu ,tunaomba na taasisi zingine ziige kutoka kwenu ili tuendelee kuwasaidia watu wenye uhitaji.




No comments