Zinazobamba

TRA YAPONGEZA WAALIMU NA WANAFUNZI KWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU SHINDANO LA VILABU VYA KODI

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Nchini Tanzania TRA Bw. Charles Kichere akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi katika mamlaka Mapato nchini Tanzania TRA Bw. Richard Kayombo wakati wa shindano la Vilabu vya Kodi lililofanyika kwenye Chuo cha Kodi Mwenge jijini Dar es salaam leo.
KAY2
Baadhi ya majaji wa shindano hilo wakiedelea na kazi yao ya kupata washindi wa shindano hilo.
KAY3
Baadhi ya washiriki kutoka shule ya sekondari ya Saint Joseph jijini Dar es salaam.

KAY4
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere ametoa pongezi nyingi  katika hotuba yake kwa waalimu ,  wanafunzi  na Wakuu wa  Idara mbali mbali za Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na  wadau wote kwa kazi nzuri ya kushiriki kwenye mashindano ya vilabu vya kodi  kwa  shule za Sekondari za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Amesema kuwa  ni matumaini yake  kuwa wanafunzi wamejiandaa vizuri na kwa kiwango cha hali ya juu katika uelewa wa masuala ya kodi na ni kutokana na jitihada zao  ndiyo maana leo wapo tayari kwa shindano. “Tunatarajia shindano hili litafanikiwa  mbali ya kuwa mlikuwa na majukumu mengine yakimasomo” amesema Kamishna Kichere.
Kamishna Kichere ameyasema  hayo leo wakati wa mashindano ya vilabu  vya kodi katika shule mbalimbali mkoani Dar es salaam na Pwani yaliyofanyika Mwenge kwenye Chuo cha Kodi  jijini Dar es salaam na kushirikisha shule mbalimbali katika mashindano hayo.
Ameongeza kuwa  Inafahamika bila kificho kuwa hakuna jambo lolote linaloanzishwa na kufanikiwa bila kuwa na walimu. Katika mashindano yanayofanyika walimu wamefanya kazi kubwa sana ya kuwaunganisha na kuwaandaa wanafunzi na shule zao.  Hongereni sana kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya. Ni mchango wenu pia katika kujenga Taifa letu.
Aidha Kamishna Kichere amewashukuru  sana wanachama wa vilabu  vya kodi  kwa kuwa mstari wa mbele katika kujiandaa na mashindano hayo ambayo yanategemewa kuleta tija katika masuala mazima ya kodi hapo baadaye 
Amewaomba walimu kuendelea kutoa msaada katika kuendeleza  vilabu hivi kwani kwa kufanya hivyo utakuwa ni mchango wao mkubwa wa kusambaza elimu ya kodi kwa taifa. TRA inaahidi kuendelea kutoa msaada na ushirikiano katika vilabu vya kodi vilivyoanzishwa na kuendelea kufungua vilabu vingine katika shule nyingi zaidi za sekondari nchini.
Amemaliza kwa kuwakumbusha  waalimu na wanafunzi wanaoshiriki katika mashindano  haya  kuwa waliyojifunza ni vyema wakayafanyia  kazi na kuwapatia wengine elimu hiyo kwa manufaa ya Taifa letu. TRA itatoa kila ushirikiano kwa shule zote ambazo zitaonyesha uhitaji wa kupata elimu ya kodi wakati wote itakapohitajika.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi katika mamlaka Mapato nchini Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo amewapongeza  walimu na wanafunzi hao kwa kazi nzuri waliyoifanya mpaka kufikia siku ya mashindano hayo yaani leo.
Bw. Kayombo amesema Vilabu vya kodi ni mkusanyiko wa wanafunzi wenye nia ya kukuza ufahamu na uelewe wa masuala mbalimbali yanayohusu  kodi katika shule za sekondari vinalenga hapa nchini ikiwa ni pamoja na  Kuandaa vijana waweze kutimiza wajibu wao pindi watakapoanza kupata mapato.
Ameongeza kwamba lengo kubwa ni Kukuza ufahamu wa masuala mbalimbali ya kodi kwa vijana, Kuandaa wataalamu wa kodi wa baadae, Kuwafanya wanachama waelewe umuhimu wa kudai risiti wanunuapo bidhaa au huduma, Kuwajengea uzalendo  vijana wawe na utamaduni wa  kulipa kodi kwa wakati.
Ameongeza kuwa  serikali inatumia kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na Kumjengea mwanafunzi uwezo wa kufikiri, kujiamaini na kuchambua kwa ufasaha masuala mbalimbali yanayohusu  kodi .
Mamlaka ya Mapato Tanzania imekuwa ikifanya mashindano haya kila mwaka tangu mwaka 2008, ambapo katika shindano la mwaka huu wanafunzi watashindana juu ya masuala mbalimbali kuhusu kodi na ukusanyaji wa risiti.
Serikali ya awamu ya tano imeweka kipaumbele katika kuhakikisha kuwa mapato ya serikali yanakusanywa kwa ufanisi na weledi hivyo basi katika shindano hilo Mamlaka ya Mapato (TRA) inatarajia  kupata washindi waliokusanya risiti nyingi katika manunuzi mbalimbali  yaliyofanyika toka kwa wafanyabiashara  katika Mikoa Dar es Salaam na Pwani, kama kauli mbiu yetu inavyosema” Ukiuza Toa Risiti na Ukinunua Dai Risiti”.
Kayombo ameongeza kuwa katika shughuli yoyote haikosi kuwa na changamoto  na changamoto ambazo tunakabiliana nazo kama TRA ni  Ufinyu wa bajeti kwa ajili ya Kutoa elimu ya kodi kwa wanachama wote ili waweze kuelewa sheria za kodi zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na Kuandaa makongamano na midahalo ambayo itawezesha wanafunzi kukutana na kubadilishana mawazo kwa ufanisi mkubwa .