Zinazobamba

Hukumu anazoweza kupewa mtu aliyeuwa bila kukusudia

Kuna aina nyingi za kesi duniani lakini kwa leo tuangalie aina ya kesi ya kuua bila kukusudia (manslaughter) maana yake na hukumu ambazo zinaweza kutolewa na mahakama kwa mtu aliyeua bila kukusudia.

Kwa mujibu wa kifungu namba 195, sura ya 16 kanuni za adhabu ndio kifungu kilichoelezea maana ya kesi ya kuua bila kukusudia na adhabu zake.

Katika  sheria  kuua  bila  kukusudia  (manslaughter)  kunatofautishwa  na  kuua  kwa  kukusudia (murder) kwenye kifungu hicho. Kuua  bila  kukusudia  ni  kuua ambako  muuaji  anatenda  kitendo hicho kinachopelekea  umauti  lakini bila dhamira, lengo au nia ya kukusudia kuua.

Wakati  kuua  kwa  kukusudia  ni  pale  mtu  anapotenda  tendo   ambalo  linapelekea  mauaji  ya  mtu   lakini  amefanya  hivyo  akiwa  amedhamiria   kuua.  Kwahiyo  haraka  utaona  kuwa  tofauti  kubwa  ya  kuua kwa  kukusudia  na  ile  ya  kuua  bila  kukusudia  ni  dhamira, nia au  lengo.

Je, utajuaje kuwa mtuhumiwa aliua bila kukusudia?
Yapo  mambo  ambayo  hutizamwa  na  mahakama ili kujua  iwapo  kulikuwa  na  dhamira  ya  kuua  au haikuwepo.  Moja  ya  jambo kubwa  ambalo  huangaliwa  ni   mazingira  kabla  ya  tukio, mazingira  wakati  wa  tukio  na  baada  ya  tukio…

Kwa  mfano  mtu A alimshambulia mtu B kwa matusi  mabaya. Mtu B akakasirika  sana, Baadae  Mtu B  akaenda  kwake  akaja na panga  na kumuua  Mtu A.  Hapa Mtu B  atakuwa  ameua  kwa  kukusudia  kwasababu   alisafiri  kutoka eneo la tukio, akatembea  mpaka  nyumbani  kwake, akatafuta  panga,  akaanza  safari  ya  kurudi,  akamtafuta  tena mtu A,  akampata  na kumshambulia hadi kumuua.

Lakini  ingekuwa  palepale  baada  ya  kushambuliwa kwa matusi akampiga  na  kumuua,  ingekuwa  kuua  bila  kukusudia kulikotokana na joto  la  hasira (heat  of  passion).

Kwahiyo  ushahidi wa mazingira ya tukio kama  hayo ndio utaifanya  mahakama  iamue  kama  mtuhumiwa  ameua  kwa  kukusudia   au  hakukusudia.

Hata hivyo, upande  unaosema  aliua  bila  kukusudia  utaleta  ushahidi  kuonesha mazingira  ya  tukio  na  upande unaosema  alikusudia  nao  utaleta  ushahidi  kuonesha mazingira  ya  kusudi, nia au  dhamira, Soma zaidi HAPA.

Je, adhabu ya mtu aliyeua kwa kukusudia na aliyeua bila kukusudia zipo vipi?
1-Adhabu ya kuua kwa kukusudia; Adhabu kwa mtu aliyeua kwa kukusudia ni kunyongwa mpaka kufa.

2-Adhabu ya kuua kwa kutokukusudia; Adhabu kwa mtu aliyeua bila kukusudia inaweza ikawa kifungo cha maisha au kifungo cha miaka 30 jela au kifungo cha muda wowote.

Hapa kwenye kifungo cha muda wowote inaweza kuwa mwezi mmoja, miwili, mitatu, sita au  mwaka, miaka mitatu hadi miaka 20.

Kwanini adhabu ya makosa ya kuua bila kukusudia ina adhabu tofauti tofauti?
Adhabu za makosa ya kuua bila kukusudia mara nyingi hutofautiana kutokana na mazingira ya tukio jinsi lilivyotokea, ushahidi uliowasilishwa mahakamani na mtuhumiwa na mwenendo wake.

Kwenye mwenendo wake hapa huangaliwa rekodi ya mtuhumiwa kama alishawahi kufanya kosa kama hilo au makosa mengine kipindi cha nyuma pamoja na tabia zake kiujumla.

Je, kuna uwezekano kwa mtuhumiwa wa kesi ya kuua bila kukusudia kupewa adhabu ya kufanya kazi za jamii (Community Service) ?

Ukweli ni kwamba kutokana na ukubwa wa tukio la kuua ni ngumu kwa mtuhumiwa kupewa adhabu kama hiyo.