Zinazobamba

SUMAYE AENDELEZA MAPAMBANO YA KUDAI DEMOKRASIA NCHINI,SOMA HAPO KUJUA

FREDERICK SUMAYE.

WAZIRI Mkuu mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Frederick Sumaye, amesema kuwapo kwa vyama vingi vya siasa hata vikiwa zaidi ya 1,000 siyo demokrasia.

Badala yake, Sumaye alisema, demokrasia hupimwa kwa uwapo wa uhuru wa habari, kujieleza na tume huru ya uchaguzi.
Amesema hayo juzi wakati akijibu baadhi ya maswali kutoka kwa washiriki wa kongamano lililofanyika mjini Geita na kuwashirikisha wadau na wanachama wa Chadema wa mkoa huo.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa “Pigania Demokrasia ya kweli inayotaka kupotezwa kwa kunyimwa uhuru wa habari wa kujieleza na kupata habari na kutoa maoni yetu.”

Sumaye alisema utawala wa sheria huzingatia na kuongozwa na katiba ya nchi ambayo kila kiongozi wa nchi huapa kuilinda na si vinginevyo na kwamba kuzuia mikutano vyama vya kisiasa pia ni kuminya demokrasia.

“Huwezi kusema nchi ina demokrasia wakati uhuru wa vyombo vya habari haupo, watu hawana haki ya kupata habari, kujieleza, hakuna tume huru ya uchaguzi na kutokuwapo kwa uwiano katika matumizi ya rasilimali za nchi wakati wa uchaguzi,” alisema Sumaye.

Kwa mujibu wa Simaye, nchi hata kama itakuwa na vyama vya siasa zaidi ya elfu moja hakuna demokrasia kwani demokrasia dhana yake ni kuwapo uhuru na nafasi sawa katika kujieleza kwa kuwa kujileza siyo uchochezi kutokana na katiba kuweka bayana kuwa kutakuwapo na uhuru wa kupata habari na kwamba kinyume chake ni dalili za woga wa watawala wasikosolewe.

Alifafanua kuwa serikali yoyote ilyoundwa kwa kupewa ridhaa na wananchi kupitia sanduku la kura ndio wenye maamuzi na mamlaka juu ya nini kifanyike na siyo vitisho na katiba kukanyagwa.

Akiwasilisha mada, mwanasheria wa kujitegemea, Bernard Otieno, alisema utawala bora ni utawala unaoendeshwa kwa mfumo shirikishi wa kuheshimu na kuzingatia katiba na sheria.

“Zipo haki za msingi anazotakiwa mwanadamu mara tu anpaozaliwa akiwa hai anatakiwa kuzipata, lakini pia zipo haki za kisheria kama vile haki ya kupata habari na kujieleza na kumiliki mali,” alisema Otieno.

KUMINYWA DEMOKRASIA

Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo kuanzia 1995, alikihama Chama cha Mapinduzi (CCM) Agosti 22, 2015 na kujiunga na mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), akidai kuminywa kwa demokrasia ndani ya chama tawala.

Desemba 14 mwaka huo, Sumaye alitangaza rasmi kujiunga na Chadema iliyokuwa imeshirikiana chini ya Ukawa na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, na kukakabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu mstaafu wa pili kujiunga na Chadema baada ya Edward Lowassa aliyefanya hivyo Agosti, 2015 na kuwa mgombea urais wa chama hicho na Ukawa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu Sumaye alizunguka na Lowassa nchi nzima katika mikutano ya kampeni.