MAASKOFU WAILIMA SERIKALI YA MAGUFULI WARAKA MZITO,SOMA HAPO KUJUA
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa
waraka uliojumuisha mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi
kutenda haki, kutokuwa na upendeleo, kuheshimu Katiba na sheria za nchi.
Pia jumuiya hiyo imewataka Watanzania kwa ujumla
kuliombea taifa na viongozi wake, ili wawe walinzi wa Katiba na sheria za nchi
kama walivyoapa.
Waraka huo ulisambazwa jana katika vyombo vya
habari, ukiwa umetiwa saini na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana
Tanzania (KAT), Dk. Jacob Chimeledya.
Wengine ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian
Tanzania (KMT), Dk. Isaac Nicodemo na Askofu Mkuu wa Kanisa la African Inland
Church in Tanzania (AICT), Silas Kezakubi.
“CCT inatoa maelekezo kwa Wakristo wa
makanisa wanachama na Watanzania wote kwa ujumla, kuendelea kulinda na
kuheshimu misingi ya haki za binadamu na kuliombea taifa na viongozi wake ili
waendelee kuwa na hofu ya Mungu na waadilifu.
“Watende haki, wasiwe na upendeleo na
waheshimu na kuwa walinzi wa Katiba na sheria za nchi kama walivyoapa,” ilisema
sehemu ya waraka huo.
CCT ilieleza pia kusikitishwa na vitendo vya
ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii na kukemea matukio ya ukatili na
yale ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
“CCT inasikitishwa na vitendo vya
ujambazi na matumizi ya silaha katika jamii yaliyofikia kiwango cha kuua askari
polisi."
Aidha, CCT inakemea matukio ya ukatili unaondelea katika
jamii.
“Yapo matukio ambayo yamedhihirisha
ushirikiano hafifu kati ya polisi na wananchi na kuendelea kujitokeza kwa
matukio yanayoashiria chuki za kidini na kikabila.
“CCT inatoa wito kwa Serikali
kuhakikisha misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa inaheshimika na utawala
wa kisheria unafuatwa,” ilisema taarifa hiyo.
Dawa za Kulevya
CCT ilisema ili vita dhidi ya dawa za kulevya
ifanikiwe, ni muhimu Serikali ikalenga kutokomeza kiini cha tatizo kwa kuwapata
wahusika wakuu wa biashara hiyo bila kujali wasifu wao na nafasi walizonazo
katika jamii.
Kutokana na hilo, CCT ilisisitiza kuwa Serikali
izingatie misingi ya sheria, haki na usawa katika kuwakamata, kuwapekua na
kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kuonea mtu wala kusukumwa na misingi
yoyote ya imani au itikadi ya mtu.
“CCT inaunga mkono vita dhidi ya
matumizi ya dawa za kulevya na viroba iliyoanzishwa na Serikali. Hata hivyo,
CCT inasisitiza kuwa ili vita hii ifanikiwe, ni muhimu sana Serikali ilenge
kutokomeza kiini cha tatizo kwa kuwapata wahusika wakuu wa biashara hii bila
kujali wasifu wao, nafasi zao wala nafasi walizo nazo katika jamii.
“Katika kufanya hivyo, ni muhimu
Serikali izingatie misingi ya sheria, haki na usawa katika kuwakamata,
kuwapekua na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kuonea wala kusukumwa na
misingi yoyote ya imani au itikadi ya mtu.
“Ni muhimu kwa Serikali kuendelea kuweka
mazingira wezeshi kwa vijana kupata ajira na kuendesha shughuli za ujasiriamali
ili kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo matumizi ya dawa za kulevya na unywaji
wa pombe kali.
“CCT inayaelekeza makanisa wanachama,
wazazi na walezi kuendelea kuwalea vijana wao katika misingi ya kidini ili
wasijiingize katika matumizi ya dawa za kulevya na pombe kali.
“Wakati huu wa Kwaresma, tunawaombea na
kuwaomba wale wote ambao kwa njia moja au nyingine wanajihusisha na dawa za
kulevya au unywaji wa pombe kali, watubu na kuyaacha maovu yao na Mungu
atawarehemu,” walisema maaskofu hao.
Hali ya Chakula
Kuhusu hali ya chakula nchini, CCT ilisema kuwa
pamoja na mvua kuanza kunyesha, Serikali na wengine wawezeshe usambazaji wa
chakula kutoka mikoa yenye ziada kwenda mikoa yenye uhaba wa chakula ili bei ya
chakula iweze kushuka.
“Tunaiomba Serikali kupitia idara yake
inayohusika, iratibu na kusaidia utekelezaji wa jambo hili, ili wananchi waweze
kumudu bei, mfano mahindi hayo yakisambazwa, bei ishuke kutoka zaidi ya Sh
100,000 ifikie angalau Sh 60,000.
“Pia tunawaomba wakulima wasitumie njaa
hii kutekeleza usemi ya kwamba ‘kufa kufaana’, hivyo kwao kipindi hiki kigumu
kwa Watanzania wengine wakakifanya kipindi cha kupandisha bei ili kupata faida
kubwa.
“Sambamba na wito huu, tunawaekeleza
wanachama wetu kupitia vitengo vya maafa na misaada ya kibinadamu, waendelee
kuwasaidia wananchi wenye upungufu mkubwa wa chakula wakipate kwa bei nafuu
kwenye maeneo yao,” ilisema.
CCT iliwataka Wakristo wote kuendelea kumwomba Mungu
ili mvua zinazoendelea kunyesha ziwe za neema na zisilete madhara.
Katika hilo, wameiomba serikali kutoa unafuu wa bei
ya gesi ya kupikia ili wananchi wengi wapunguze au kuachana kabisa na matumizi
ya kuni na mkaa.
Elimu
CCT ilisema pamoja na nia njema ya Serikali kutoa
elimu bure, lakini iangalie masilahi ya walimu na kuwe na mpango mkakati
unaotekelezeka wa kuimarisha miundombinu ya kufundishia.
“Serikali haina budi kuendelea
kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu dhana ya elimu bila malipo, ili
kuepusha migogoro inayokabili sekta ya elimu kwa dhana hiyo kutoeleweka kwa
vizuri kwa baadhi ya wananchi.
“Pia mabadiliko ya mitaala na miongozo
mingine ya kufundishia ya mara kwa mara imekuwa ikiathiri elimu ya Tanzania kwa
kila awamu ya uongozi na kuwafanya wahitimu wetu kukosa ushindani kikanda na
kimataifa,” ulisema waraka huo.
Kupitia waraka huo, maaskofu waliishauri Serikali
kuwa na será ya elimu isiyobadilika badilika kila uongozi mpya unapoingia
madarakani.