SUMAYE AFAGILIWA NA WASOMI,WENGI WAMTABILIA MAKUBWA NDANI YA CHADEMA,SOMA HAPO KUJUA
Wasomi nchini wamesema iwapo Waziri Mkuu mstaafu,
Frederick Sumaye atakuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, atasaidia
kukijenga chama hicho cha upinzani nchini, kuanzia ngazi ya chini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema jana kuwa
Sumaye ambaye juzi alirejesha fomu ya kuwania nafasi hiyo, katika ofisi za
kanda hiyo Dar es Salaam, akitumia uzoefu alionao kiuongozi, atakuwa msaada kwa
chama hicho.
Walisema uamuzi huo umeonyesha kuwa hakuhamia
Chadema kwa masilahi binafsi. Profesa George Shumbusho wa Chuo Kikuu cha Mzumbe
alisema: “Inaonekana (Sumaye) ana lengo la kusaidia upinzani ukue. Kwa
mchango na uzoefu wake serikalini ataisaidia sana Chadema maana chama lazima
kiwe na nguvu kuanzia ngazi ya chini.”
Sumaye ndiye Waziri Mkuu pekee katika historia ya
Tanzania kushika wadhifa huo kwa miaka 10 baada ya kuwa msaidizi wa Rais
mstaafu, Benjamin Mkapa kati ya mwaka 1995 hadi 2005.
Agosti mwaka jana, Sumaye aliyekuwa kete muhimu
katika kampeni za aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa kutokana
kuikosoa Serikali na kuwataka Watanzania kutoichagua CCM, alitangaza kuachana
na chama hicho tawala na kujiunga na upinzani.
Shumbusho alisema ameonyesha kuwa yeye siyo aina ya
wastaafu wanaopenda sifa na hakwenda kusaka ulaji Chadema huku akibainisha nchi
ikiwa na upinzani imara, chama kilichopo madarakani hugangamala.