BAVICHA WABADIRI GIA ANGANI,NI KUHUSU MKUTANO MKUU WA CCM,SOMA HAPO KUJUA
Viongozi wa Bavicha wakizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani |
BAADA ya kutakiwa kuachana na mpango wa kuzuia
mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha) limeamua kubadili mbinu, anaandika Faki Sosi.
Kwa zaidi ya wiki tatu sasa,
Bavicha na Jeshi la Polisi wamekuwa wakivutana baada ya kuwepo kwa zuio la
mikutano ya siasa ya wazi na ndani lililotolewa na polisi pia Rais John
Magufuli.
Leo
Bavicha wameeleza kusitisha dhambira yao ya kuzuia mkutano huo kwa heshima
maagizo ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa chama hicho taifa aliyewataka kuachana
na mpango huo.
Akizungumza
katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam, Patrobas Katambi,
Mwenyekiti wa Bavicha Taifa amesema kuwa, pamoja na kukubaliana na ombi hilo
lakini bado wanaamini kuwa, mkutano wa CCM utakaofanyika tarehe 23 Julai mwaka
huu ni haramu.
“Tutakuja
na mpango mbadala utakaoratibiwa baada ya mkutano wa kamati tendaji ya chama
utakaofanyika tarehe 20 Julai Mwaka huu. Tunasema ipo haja kwa serikali
kutangaza kufuta vyama vya siasa na kibaki chama cha CCM kuliko kuvunja sheria
na kuipendelea,” amesema Katambi na kuongeza kuwa “kwa sasa ni mapema kutaja
mpango huo.”
Hata
hivyo Bavicha wamelitupia lawama Jeshi la Polisi nchini kwamba, haliheshimu
haki wala utawala wa sheria na linaweza kuiingiza nchi matatani wakati wowote.
Wakati
Bavicha wakisema hivyo, jeshi hilo limeeleza kuwa, mtu ama chama chochote
kitakachokwenda kinyume na maelezo yao, watapambana nacho/naye.
Kauli
hizi zinatoka ikiwa ni baada ya Jeshi la Polisi kupiga marufuku mikutano ya
hadhara ya kisiasa ya ndani na nje nchi nzima kauli ambayo ilitanguliwa na ile
ya Rais John Magufuli kwamba, siasa zisifanyika mpaka kwenye uchaguzi mkuu wa
mwaka 2020.
Patrobas
Katambi, Mwenyekiti wa Bavicha Taifa akizungumza na waandishi wa habari hii leo
Makao Makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam amedai kuwa, jeshi hilo limekuwa
likilinda maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hata kama kinatenda mambo yaliyo
kinyume na sheria na Bavicha haitavulia upendeleo huo.
“Polisi
wa nchi hii wapo radhi wafe wao lakini CCM isiguswe na waendelee kuwa
madarakani. Uko wapi usawa wa kidemokrasia? Uko wapi weledi wa utendaji wa
jeshi letu la polisi,” amehoji Katambi.
Katambi
amesema kuwa, zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa limelenga vyama vya
upinzani tu ambapo CCM na viongozi wake wa ngazi mbalimbali wanafanya mikutano
ya hadahara bila zuio lolote la polisi.
“Tunayo
taarifa ya baadhi ya mawaziri na wabunge wa CCM kuwa wanafanya mikutano ya
hadhara katika majimbo mbalimbali hapa nchini, na tunazo picha za matukio hayo
kama ushahidi, polisi wanataka tuamini kuwa wanatumika?” amesema.