UDHAIFU WA KIKWETE SIO UIMARA WA RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
MPAKA sasa, sifa
kuu ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli ni kujenga
ufuasi wa kushangiliwa kwa kila jambo, anaandika Gululi Kashinde.
Washangiliaji wako kila kona. Wapo kwenye
mitandao ya kijamii, wapo mitaani na hata kwenye mikusanyiko ya watu.
Kimsingi, uimara wa Rais Magufuli unaoonekana kuwepo, unatokana
na udhaifu wa awamu iliyopita.
Shangwe na vigelegele vinavyopigwa leo kwa Rais Magufuli,
zinatokana na mchoko wa muda mrefu waliokuwa nao wananchi, hususan katika
kipindi chote cha miaka kumi ya utawala wa rais aliyepita, Jakaya Kikwete.
Kinachofanyika sasa, ni ukali na kujenga hofu kwa watumishi wa
umma. Serikali hii imeanza kujenga kasumba mbaya kwa wananchi.
Serikali inajikosha na kujenga hisia bandia kwa wananchi kwamba,
matatizo yao hayatokani na serikali yenyewe, bali watendaji wa serikali.
Ni hatari sana, kwa serikali kuanza kujenga hisia za
uchonganishi kwa watendaji dhidi ya wananchi.
Orodha ya matukio ya namna hii ni ndefu. Leo madaktari na
wauguzi hawako salama kazini. Baadhi ya maeneo wameanza kutishia kogoma kutoka
na vitisho na vipigo wanavyopata kutoka kwa ndugu na jamaa wa wagonjwa.
Ni hatari sana kumwaminisha na kuhadaa wananchi kuwa, huduma
mbovu za kijamii wanazopata, hususan katika hospitali zetu, zinatokana na
madaktari na wauguzi kuiba dawa.
Ukiwasikiliza wauguzi na madaktari wanasema, “huwezi kuiba dawa
ambazo hazipo.” Serikali inawachonganisha watendaji wake kwa wananchi ili
ipumue. Sijawahi kuona!
Kuna mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa kuhusu
mshahara wa rais. Kama kawaida, Rais Magufuli anamiminiwa sifa kemkem kwa
kuweka mshahara wake hadharani.
Yaleyale, wanaoshangilia na kupiga vigelegele, wanamulinganisha
Rais Magufuli na mtangulizi wake, Kikwete. Ukweli ni kwamba, udhaifu wa Kikwete
hauwezi kuwa uimara wa Rais Magufuli.
Uzalendo wa rais haupimwi kwa kutangaza mshahara wake. Bali
tunahitaji rais asiyependa kupiga dili wala kufanya biashara akiwa ikulu.
Hatutaki rais anayeweza kujificha kwenye kivuli cha dola ili
kudhoofisha wapinzani wake na wanaokosoa serikali.
Kasumba inayojengwa kwa kasi hivi sasa ni kwamba, yeyote
anayekosoa na kutoa maoni mbadala, anaonekana kama mkorofi na siyo mzalendo.
Uzalendo siyo uzuzu wa kukaa kimya. Wala uzalendo haupimwi kwa
kukubali kila kitu kinachosemwa na watawala.
Katika taifa ambalo ubabe unaitwa ujasiri na udhaifu wa
kutofuata sheria na taratibu, unaitwa uungwana, huko ni kutengeneza wazalendo
wa kuchonga.
Baada ya sakata la Zanzibar, hasa kwenye vituko vya kuamua
kurejea uchaguzi Machi, 20, 2016, na Rais Magufuli akasema hahusiki na wala
hana uwezo wa kuingilia utata ulioibuka uchagzi wa visiwa hivyo, vikiwa sehemu
ya muungano wa Tanzania, inaonekana nchi inaendeshwa kibabe, haifuatwi matakwa
ya wananchi na kiongozi mkuu anakubali kuisigina Katiba.
Pamoja na hilo la Zanzibar kusimamiwa kibabe na hatimaye kupita,
bado Rais Magufuli amebakiza changamoto kadhaa.
Kwanza, mchakato uliokwama wa Katiba Mpya. Wapo baadhi ya
viongozi waandamizi katika serikali hii ya Rais Magufuli wanaojipanga kimkakati
kukwamisha hoja ya kufufua mchakato wa katiba mpya.
Nilimsikia waziri mmoja mwandamizi akisema, “wananchi mahitaji
yao siyo Katiba Mpya, bali huduma bora za kijamii na kuboreshewa maisha yao.”
Hawa ndio wanaomzunguka Rais Magufuli.
Hawa ndio washauri wakuu wa rais. Rais Magufuli asijifiche
kwenye koti la washauri. Ajifunze kwa mtangulizi wake. Mambo yakienda kombo
anayemiminiwa shutuma ni rais, siyo washauri.
Pili, kivuli cha Kikwete ndani ya Serikali ya Magufuli.
Kinachoelezwa kuwa ni “utumbuaji wa majibu” ndani ya awamu hii ya tano,
kinaenda sambamba na upangaji safu wa awamu hii.
Rais Magufuli anataka kujenga safu yake mpya atakayofanya nayo
kazi. Kikwazo pekee ni kuwa, huwezi kupata safu mpya bila uwepo wa chembechembe
za masalia ya Kikwete.
Mzee mmoja mashuhuri ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameonya
kuwa, kama Rais Magufuli atapewa kuwa Mwenyekiti wa CCM, basi asiwategemee
wanaCCM kumsaidia katika harakati zake za “utumbuaji majipu”.
Sababu ni kwamba, baadhi ya wabunge wa CCM ndio wametuhumiwa na
hata kufikiswa mahakani kwa mashitaka ya rushwa.
Kwa hiyo, Bunge haliwezi tena kuwa chombo cha kuibua uozo na
tuhuma za rushwa, kwa sababu sehemu ya Bunge hilo, liko kwenye kashfa. Mnara wa
kutunga sheria unapotuhumiwa, usitegemee mijadala mikali ndani ya bunge kuhusu
ufisadi wala tuhuma zingine zinazofanana na hizo.
Hivyo, Rais Magufuli hawezi kupata msaada kutoka kwa wabunge wa
CCM ndani ya Bunge. Na pia sasa mhimili wa Bunge, umepoteza sifa za kuwajadili
mafisadi.
Huu ni mkwamo mwigine kwa Rais Magufuli, hususan kwa wabunge wa
CCM wenye idadi kubwa na kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi ndani ya Bunge, ambao
una maslahi ya chaa chao na serikali.
Rais Magufuli mwenyewe anaweza kuwa changamoto. Hulka yake ya
kutopenda kuamini kila mtu na kusimamia uamuzi wake mpaka mwisho hata kama siyo
sahihi, inaweza kuchochea changamoto zaidi.
Hulka ya kutoamini kila mtu ina madhara yake. Hasara yake ni
kujenga watendaji na wasaidizi wasiojiamini, wao wanasubiri kauli ya rais,
ndipo wachangamke na kutenda kwa uoga.
Orodha ya matukio ya namna hii ni mengi. Wapo wanaoogopa kufanya
uamuzi ambao upo ndani ya uwezo wao, kwa mujibu wa sheria na taratibu, lakini
hawafanyi hivyo kwa hofu ya kukosea na kumkera bwana mkubwa.
Matokeo yake kazi haziendi mpaka tamko la Ikulu, tena kutoka kwa
mkuu wa nchi liwafikie. Hawawezi kuwa wabunifu na kuamua ili kazi ziende kasi
na maendeleo ya wananchi kupatikana.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni