Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Aeleza matumaini yake Kutokomeza malaria Katika Bara la Afrika
RAIS
mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema, ana imani kwamba
kupitia ushirikiano uliopo baina ya serikali mbalimbali barani Afrika,
mashirika ya kimataifa, makampuni binafsi na kila mtu katika nafasi
yake, ugonjwa wa malaria unaweza kumalizwa kabisa.
Kikwete
alionesha matumaini hayo juzi wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 10
tangu kuanzishwa kwa jitihada za kuutokomeza ugonjwa wa malaria (Malaria
no more) zilizoanzishwa na Ray Chambers akishirikiana na Peter Chernin.
Katika
hafla hiyo, Kikwete alitunukiwa tuzo ijulikanayo kama White House
Summit Awards ikiwa ni kutambua uongozi wake, kujitoa kwake na kubwa
zaidi kusimamia uanzishwaji wa muungano wa viongozi wa Afrika dhidi ya
malaria (ALMA), muungano ambao hadi sasa una viongozi 49.
Wengine
waliotunukiwa tuzo hiyo ni Ray Chambers na Sumitomo Chemical. Akijibu
swali la nini anadhani kimechangia katika kupunguza idadi ya vifo
vitokanavyo na ugonjwa wa malaria, Kikwete alisema zipo sababu kadhaa,
lakini kubwa ni utashi wa kisiasa wa kusimamia na kuongoza mapambano
dhidi ya ugonjwa huo.
Akawaeleza
wageni zaidi ya 250 walioalikwa wakiwa ni wawakilishi wa makapuni na
mashirika mbalimbali yanayochangia juhudi za kuukabili ugonjwa wa
malaria kwamba, upatikanaji na usambazaji wa dawa sahihi za kutibu
ugonjwa wa malaria, utengenezaji, usambazaji na matumizi ya vyandarua
vyenye viuatilifu na unyunyiziaji wa dawa za kuua mazalia ya mbu ni
mambo ya msingi ambayo yamechangia katika kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni