KANISA LA KKKT LAPATA PIGO KUBWA,MCHUNGAJI WAKE ATUPWA JELA KWA WIZI,SOMA HAPO KUJUA
Moshi. Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Rauya, Zawadiel Maruchu amehukumiwa
kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la wizi wa kuaminiwa.
Usharika aliokuwa
anahudumu mchungaji huyo upo Mambo katika Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la
Dayosisi ya Kaskazini.
Hukumu hiyo ilitolewa
juzi na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Himo – Moshi, Shaban Mkude baada ya
kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Kesi hiyo ya jinai namba
417/2015, ilifunguliwa na mlalamikaji Judith Matemba, akimtuhumu mchungaji
Maruchu kwa kujipatia Sh8.3 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Kosa hilo ni kinyume na
Kifungu namba 304, Sura ya 16 ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marejeo na
Bunge mwaka 2002, kosa ambalo adhabu ni kifungo cha miaka mitatu. Awali,
mwendesha mashtaka, Koplo Patrick Mgiriama alidai mahakamani kuwa mshtakiwa
alitenda kosa hilo Septemba 16, 2011 akimshawishi Judith anunue kiwanja eneo la
Njiapanda ya Himo.
Siku hiyo mshtakiwa
alimfuata mlalamikaji dukani kwake na kumshawishi kuwa kuna kiwanja kinauzwa
karibu na Sekondari ya Muungano kwa Sh8.3 milioni.Hakimu alisema mshtakiwa
ndiye aliyewachukua mlalamikaji na mumewe na kwenda kuwaonyesha kiwanja hicho
na kwa vile mshtakiwa ni kiongozi wa kiroho alimwamini na kukubali kukinunua.
Makubaliano ya mauzo hayo yalifanyika nyumbani kwa mchungaji na baada ya
kukabidhiwa fedha hizo, alizifanyia sala fupi na kuahidi kumpelekea muuzaji
ambaye alimtaja kuwa ni Boniventura Kilawe.
Hata hivyo, ilibainika
baadaye kuwa kiwanja hicho kilikuwa kinamilikiwa na mtu mwingine aliyekuwa na
hati za umiliki na jitihada za mlalamikaji kutaka arudishiwe fedha zake
hazikuzaa matunda. Hakimu Mkude alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande
zote mbili na kuuchambua, alimtia hatiani mshtakiwa huyo kwa kosa hilo na
kumhukumu kifungo cha mwaka mmoja jela. Hata hivyo, kabla ya kutolewa kwa
hukumu hiyo, mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa maelezo kuwa anategemewa
na familia, ana matatizo ya kiafya na ni kiongozi wa kiroho.
Baada ya kusikiliza
maombi ya mchungaji huyo, hakimu alisema ameyazingatia hivyo anamhukumu kifungo
cha mwaka mmoja jela na atakapomaliza alipe fedha hizo.
Jana, mlalamikaji katika
kesi hiyo alisema baada ya kutolewa kwa hukumu, ndugu wa mfungwa huyo
walitafuta fedha hizo na tayari amelipwa hivyo yatakayoendelea yeye hayamhusu
tena.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni