CCM,UKAWA WATIA "DOA" MDAHALO WA URAIS
Wagombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM) Dk John Magufuli, pamoja na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo (Chadema), wameutia doa mdahalo wa kiti cha urais baada ya kushindwa kushiriki mdahalo maalum wa
wagombea urais ulioandaliwa na Taasisi ya Twaweza pamoja na wadau
wengine.
Mdahalo
huo ambao umefanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam leo, ulirushwa moja kwa moja na kituo cha
televisheni cha Star TV. Anna Mghwira kutoka Chama cha ACT-Wazalendo na
Chief Lutasola Yemba wa ADC na mgombea kutoka CHAUMMA, Hashim Rungwe
ndiyo wagombea pekee wa urais waliopewa mualiko rasmi na kushiriki
mdahalo huo.
Hata
hivyo, Rungwe alifika wakati mdahalo huo ukiwa unaelekea ukingoni
ambapo awali ilitaarifiwa kuwa angefika kwa kuchelewa kwa kuwa wakati
mdahalo umeanza yeye ndio alikuwa akiwasili Uwanja wa ndege wa Julius
Nyerere akitokea Mtwara.
Katika
mdahalo huo, maswali mbalimbali yaliulizwa ikiwemo dhana nzima ya
mabadiliko ambayo awali ilikuwa ikitumiwa na Chadema kisha kuenea kwenye
vyama vingine, imepata tafsiri tofauti kutoka kwa wagombea urais wa
ACT-Wazalendo Anna Mghwira na Chief Yemba wa ADC.
Kwa
mujibu wa Mghwira, dhana ya mabadiliko katika ACT-Wazalendo ni hoja
mbadala inayolenga kushughulikia matatizo ya jamii. Alisema
ACT-Wazalendo imebuni mikakati madhubuti wa kuongeza uzalishaji kupitia
rasilimali za nchi kama vile misitu, madini na uwekezaji kwenye kilimo.
“Matumizi
bora ya rasilimali na uwekezaji katika kilimo vitasaidia kuongeza pato
la taifa na hivyo itarahisisha utoaji wa huduma bora za jamii kama vile
elimu na afya,” alisema Mghwira.
Kwa
upande wake, Chief Yemba alisema dhana ya mabadiliko kwa mujibu wa ADC
ni kuondoa maradhi, ujinga na umasikini. Alisema mabadiliko siyo
kuiondoa CCM madarakani na kisha kuiongoza nchi kwa misingi ileile ya
CCM.
Kuhusu
Muungano, Chief Yemba alisema ADC itapitia kero zote ili Muungano uweze
kutoa haki sawa kwa watu wote tofauti na ilivyo sasa. Alisema Muungano
unapaswa kusimamia na kutekeleza hoja ya haki sawa kwa wote kama vile
kutoa huduma za jamii kwa usawa kwa pande zote za Muungano.
“Sisi
ACT-Wazalendo tunasema Muungano ni lazima utokane na ridhaa ya wananchi
kikatiba tofauti na ilivyo sasa. Hoja za wananchi kudai serikali ya
Tanganyika au Zanzibar yenye mamlaka kamili, zinaonyesha wazi kwamba
Muungano tulionao unahitaji marekebisho ili wananchi wenyewe waridhie,” alisema Mghwira.
Mgombea
urais kupitia Chama cha TLP, Maxmilian Lyimo, pamoja na kwamba hakuwa
mmoja wa wazungumzaji kwenye mdahalo huo, alipata fursa ya kujibu baadhi
ya hoja za wananchi kama vile afya bora. Alisema serikali yake
haitafanya dawa kweye hospitali za umma kuwa bidhaa adimu kama ilivyo
sasa.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni