TAARIFA KAMILI KIFO CHA MUFTI SIMBA,NI SIMAZI NA VILIO KILA MSIKITI SOMA HAPO KUJUA
![]() |
| Sheikh Mkuu, Mufti Issa Shaaban Simba (kushoto) akiwa na Rais Jakaya Kikwete enzi za uhai wake |
NI mstuko. Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti
Shaban bin Simba, ameaga dunia asubuhi ya leo, Jumatatu 15 Juni 2015, katika
hosptali ya TMJ, jijini Dar es Salaam.
Hakuna shaka kuwa
kifo cha Sheikh Simba kitakuwa pigo kubwa kwa waislamu na taifa kwa ujumla
wake. Mufti Simba alichaguliwa kuwa Mufti mwaka 2002.
Uchaguzi wa Mufti ulifanyika kutokana
na kifo cha Marehemu Hemed Bin Juma bin Hemed. Kinyang’anyiro cha uchaguzi ule
kilikuwa na ushindani mkali kati ya Shekh Simba na Shekh Sulemani Gorogosi.
Sheikh Gorogosi alifariki dunia 27 Juni 2009.
Uchaguzi
ulifanyika katika ukumbi wa Chuo Cha Biashara (CBE) mjini Dodoma. Mara baada ya
kutangazwa mshindi, Sheikh Simba aliwaambia wajumbe wa mkutano mkuu kuwa
“vichwa visivyosikia nitavipiga marungu.”
Bila shaka, si wengi
waliomuelewa na wala si wengi walioelewa kauli halisi ya Mufti Simba. Wengi
walikuwa gizani.
Lakini miaka mitano
tangu Shekh Simba achaguliwe kushika nafasi hiyo, wengi wameanza kumuelewa.
Kwamba kauli yake ya “Vichwa visivyosikia nitavipiga marungu,” iliwalenga “wanaolivuruga”
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Wakati huo,
machoni mwa wengi, BAKWATA ilionekana kama chombo kilichopotea njia. Asilimia
kubwa ya waislamu walikuwa hawaikubali.
Wengi waliona baraza
hilo kama chombo cha serikali na chama tawala-CCM. Baadhi yao walikuwa wanasema
waziwazi kwamba BAKWATA imeingiliwa na serikali.
Kipaumbele chake
hakikujulikani machoni mwa waislamu wengi. Maswali kama, BAKWATA inakwenda wapi
au Baraza litafika kweli, yalikuwa yakisikika kila kona. Mapambano kadhaa yalianzishwa
kuipinga BAKWATA na viongozi wake.
Kilikuwa ni kipindi
cha harakati na hatua za kuikataa BAKWATA zilifika mbali. Wanaharakati kadhaa
walihubiri ubaya wa Baraza na kile lilichokiita “ndoa yake na serikali.” Hicho
ndicho chanzo au kichocheo cha “mauaji ya Mwembechai.”
Kulikuwa na hata
madai kwamba baadhi ya waislamu walipanga mapinduzi dhidi ya uongozi wa Baraza.
Mihadhara na makongamano vilifanyika usiku na mchana.
Kila pembe ya nchi
waislamu walisimama kulaani Baraza na kuituhumu serikali kwamba inawalinda
viongozi wake. Misikiti kadhaa ilianzisha harakati kwa madai kwamba BAKWATA
imeshindwa kuutetea uislamu na waislamu kwa ujumla.
Wanaharakati
mbalimbali walichipuka; wengine wakiwa na dhamira ya kweli na wengine wakiwa
waganga njaa. Baadhi yao wanafahamika hata kwa majina na matendo yao.
Wote hawa walikuwa na
madai yanayofanana kwamba BAKWATA imemezwa na serikali na imeshindwa kuutetea
Uislamu.
Hata hivyo, watu makini
waliyadharau madai hayo baada ya kuwapima watoa madai na matendo yao. Wengi
walijua tangu awali kwamba BAKWATA haikuingiliwa na serikali wala waumini wa
dini nyingine; imeingiliwa na waislamu wenyewe.
Ni wale waliokuwa
wanaitumia BAKWATA kujinufaisha. Baadhi yao wangalipo hadi sasa, lakini wengi
wameondolewa.
Hakuna aliyejua au
hata kufikiri kwamba Mufti Simba angeweza kuwang’oa ndani ya BAKWATA; baadhi ya
viongozi walionekana kuwa kikwanzo kwa maendeleo ya uislamu.
Watu kama Ali
Mubaraka, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya BAKWATA, Mussa Hemed,
Naibu Katibu Mkuu Dini, Abas Kihemba na wengineo tayari walikuwa wameweka
mizizi yao ndani ya baraza hilo.
Wapo waliondoka wenyewe baada ya kuona mambo yanakwenda kombo,
lakini wapo wengi pia ambao wameondoka kwa kung’olewa na kimbuga cha Mufti
Simba.
Kwa hakika, Shekh
Simba amekuwa simba kweli. Amejitahidi kurudisha hadhi na heshima ya baraza
hilo mbele ya jamii. Amefanikiwa japo si kwa kiasi kikubwa kurudisha umoja na
mshikamano miongoni mwa waislamu.
Tayari sasa baadhi ya
waislamu wanalikubali baraza lao. Wengi sasa wanajua kwamba adui yao mkubwa si
serikali, wala madhehebu mengine, bali waislamu wenzao.
Na hili
linathibitika sasa wakati mgogoro unaofukuta kati ya mfanyabiashara Yusuf Manji
anayemiliki kampuni ya Quality Group na baadhi ya waislamu wakiongozwa na
mwanaharakati mahiri, Shekh Khalifa Khamisi. Kiwanja kinachogombewa ni Na.
311/1 kilichopo Kitalu T Chang’ombe, Dar es Salaam.
Taarifa zinasema
kiwanja hicho kilimilikishwa kwa kampuni ya Quality Group na baadhi ya
waliokuwa wafanyakazi wa BAKWATA, ambao tayari Mufti amewashughulikia.
Hadi sasa, haijulikani
ni kiasi gani wale “wasaliti” walilipwa kwa kazi hiyo. Linalofahamika ni kwamba
watendaji hao, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Abass Kihemba,
walifukuzwa kazi kwa madai ya kukiuka maadili ya kazi yao.
Hicho ndicho
chanzo au kichocheo cha harakati na malalamiko ya sasa yanayoongozwa na Shekh
Khalifa Khamisi. Lakini kwamba aliyemilikishwa na waliomilikisha, wote ni
waislamu, ni jambo linalodhihirisha kuwa BAKWATA na uislamu havivurugwi na
serikali, bali na waislamu wenyewe.
BAKWATA ni moja ya
taasisi ya kidini nchini iliyopata bahati ya kumiliki mali na vitegauchumi
vikubwa. Mwaka 1968 ilimilikishwa na serikali mali za iliyokuwa Taasisi ya
Waislamu ya Afrika Mashariki (East Afrika Muslim).
BAKWATA ilirithi
majumba, pamoja na vitegauchumi mbalimbali kwa dhamira kuendeleza uislamu.
Bahati mbaya hayo hayakufanyika. Kila mmoja anafahamu kwamba kama BAKWATA
ingetumia mali na rasilimali zake vizuri, leo ingekuwa mbali kimaendeleo.
Kama raslimali zake zingetumika vizuri, waislamu wangekuwa juu.
Wangepata elimu bila kutegemea msaada mkubwa kutoka kwa serikali. Na hata
malalamiko yanayoenezwa sasa kwamba serikali imewasahau waislamu yasingesikika.
Lakini bahati mbaya ni kwamba waliopewa dhamana ya kusimamia mali
na rasilimali za waislamu ndiyo haohao waliogeuka na kuzitafuna. Wakati
madhehebu mengine yako katika mbio kali za maendeleo, bado BAKWATA inatambaa.
Angalia madhehebu
mengine yanamiliki Hospitari za rufaa (Bugando-Mwanza na KCMC-Moshi), BAKWATA
imeishia kumiliki zahanati. Wakati madhehebu mengine yanamiliki vyuo vikuu, kwa
mfano Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Iringa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Augustine – Nyegezi, Mwanza, BAKWATA imeishia kumiliki sekondari.
Kibaya zaidi, hata
hizo sekondari na shule za msingi ilizonazo zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa
walimu. Nyingine hazina vitendea kazi, vikiwamo vitabu vya ziada na kiada; na
nyingi zinaongoza kwa matokeo mabaya katika mitihani ya taifa.
Hata chuo kikuu
pekee cha Morogoro (Muslim University of Morogoro), ambacho kilianzishwa miaka
miwili iliyopita kwa msaada wa serikali, tayari kinayumba. Chuo kinakabiliwa na
uhaba mkubwa wa walimu na ucheleweshaji mishahara kwa wafanyakazi.
Hakina mitaala ya kutosha na wala hakina vitendea kazi vingine
muhimu. Kwa kweli ni “bora chuo” na wala si chuo bora. Yapo madai kwamba hata
mandhari ya chuo kwa sasa hayavutii kama kilivyokuwa wakati kikiwa chini ya
Shirika la Umeme TANESCO.
Kwa hisani
ya mwanahalisi oline

No comments
Post a Comment