EXCLUSIVE-UKAWA NI MBELE KWA MBELE,WAJA 'FOMESHENI'KALI,WAGAWANA KILA UPANDE WA NCHI,SOMA HAPA KUJUA

Dar/Mikoani. Katika kile kinachoonekana kuendelea kujiimarisha
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) vimegawana maeneo mbalimbali nchini vikifanya mikutano ya hadhara na
mafunzo kwa viongozi wake ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa ushindi.
Ukawa unaundwa na
vyama vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Chadema kilianza
ziara zake mikoani wiki zilizopita baada ya kuzindua mkakati wake uitwao
‘Hakuna kulala, Hakuna kula, Mpaka Kieleweke’ nchi nzima wakati timu ya
NCCR-Mageuzi ikiweka kambi mkoani Kigoma kwa kile ilichokiita kuimarisha
majimbo ya kimkakati.
Sanjari na
vyama hivyo, CUF tangu juzi kiliingia katika moja ya ngome zake, mkoani Mtwara
pamoja na mipango mengine ya kiushindi, kinahamasisha wananchi kujitokeza
kujiandikisha kupiga kura.
Jitihada za
Ukawa kuzunguka mikoani zinakuja ikiwa ni majuma kadhaa tangu Chama cha
Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Katibu Mkuu wake Abdulrahman Kinana kilipomaliza
ziara ya kujiimarisha na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka
2010.
Pia, ziara hizo
ziligongana na zile za Chama cha ACT - Wazalendo zilizosababisha Chadema na
chama hicho kipya kugongana Butiama.
ACT - Wazalendo
kinachoongozwa na Zitto Kabwe kilihitimisha ziara yake ya kimkakati katika
mikoa tisa inayoonekana kuwa ngome ya CCM, wiki iliyopita wilayani Bariadi,
Shinyanga na kuvuna wanachama zaidi 6,000 katika mikoa hiyo.
NCCR-Mageuzi
ipo Kigoma
Katibu Mkuu wa
NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema jana kuwa Ukawa ina mikakati inayofanana
ndani ya vyama vyao ya kuhakikisha inajiimarisha kisiasa nchi nzima ili ishinde
Uchaguzi Mkuu.
Alisema siku 10
zilizopita, timu ya NCCR ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti - Zanzibar, Haji Hamis
Hamad ilianza ziara Kigoma kuhakikisha majimbo ya mkoa huo yanaendelea kuwa
ngome yake.
“Kigoma nzima ina
majimbo yetu ya kimkakati na Ukawa wameshatukabidhi sasa kilichobaki ni kufanya
‘political management’ (usimamizi wa kisiasa) katika kiwango kinachotakiwa.
“Katika kikosi
hicho, pia wamo Katibu Mwenezi, David Kafulila, Katibu Mkuu Mstaafu, Samuel
Ruhuza na Kamishna wa Kagera, Peterson Mshenyela na wengineo,” alisema
Nyambabe.
Alisema baada ya
kumalizika ziara katika mkoa huo viongozi hao wataelekea Kagera kwa kuanzia
majimbo ya Ngara na Nkenge, maeneo ambayo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
anaendelea kumwaga ‘cheche’.
Kinachoendelea
katika ziara hizo ni kama mashambulizi ya ‘bandika bandua’ na kuzuia
mparaganyiko ndani ya vyama hivyo ambao unaweza kutokea baada ya kuanza kwa
mchakato wa kugawana nafasi za udiwani na ubunge.
Chadema
kila kona
Chadema,
inayoendelea na utoaji wa mafunzo ya uongozi bora kwa viongozi wa ngazi zote na
makada waliotia nia ya kugombea na mikakati mingine ya ushindi, viongozi wake
wa juu wametawanyika maeneo tafauti katika kanda zake 10 za kiutendaji.
Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willbrod Slaa aliyekuwa Morogoro alieleza kuwa Tanzania kwa sasa
inasifika nje ya nchi kwa uvunjifu wa haki za binadamu.
Akizungumza
wakati wa mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja cha
Ndege, Manispaa ya Morogoro juzi, Dk Slaa alisema katika kipindi cha miaka
mitano, utawala wa Rais Jakaya Kikwete umekuwa na matukio mengi ya uvunjaji wa
haki za binadamu.
Alisema hivi
karibuni alikuwa Marekani kwa ziara maalumu na huko alihojiwa na waandishi wa
habari katika kituo kimoja cha redio juu ya masuala ya utawala bora nchini.
Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu akiwa mkoani Rukwa alisema CCM
imepoteza baraka za Mungu kiasi cha kushindwa kujua mgombea wake wa urais mpaka
sasa, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya chama hicho.
Mwalimu
aliyekuwa akizungumza kwenye Ukumbi wa Libori Mjini Sumbawanga, alisema
viongozi wanaotokana na Chadema wapaswa kuwa tayari kusimamia haki kwa gharama
zozote, kukataa rushwa na kupunguza kero kwa wananchi na kuwaonya wasije
wakaufanya utawala wa Chadema kuwa kama wa CCM ambayo inayumba.
“ Tuna miezi
mitatu imesalia tuanze kampeni, lakini mpaka sasa CCM haijamjua mgombea wake,
lini imewahi kutokea? Mungu amewachanganya kama wajenzi wa karavati,” alisema
Mwalimu ambaye baada ya mkutano huo aliendelea na ziara yake mjini Makambako,
Njombe.
Mwalimu alionyesha kushangazwa na baadhi ya wafuasi wa Chadema
kujiunga na chama cha ACT – Wazalendo na akakiita kuwa ni chama cha msimu
ambacho kitapotea baada ya Uchaguzi Mkuu.
Akiendelea na ziara yake mkoani Kagera, Mbowe alisema kusuasua
kwa uandikishaji wa wapigakura ni kiashiria cha uvunjifu wa amani inayotokana
na hofu ya CCM kuangushwa Oktoba.
Akiwahutubia wakazi wa Mji wa Bukoba juzi katika Uwanja wa
Uhuru, Mbowe alisema nchi inaweza kuingia katika machafuko endapo litakuwapo
jaribio lolote la kuahirisha Uchaguzi Mkuu kama upigaji kura wa Katiba
Inayopendekezwa ulivyoahirishwa.
Alisema uchaguzi siyo suala la dharura na kila hatua inatakiwa
kuwekwa wazi ili kuondoa hofu iliyoanza kujengeka kutokana na kubakia miezi
michache kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Profesa
Lipumba, Mtwara
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa endapo
Wapinzani wataingia madarakani, kazi ya kwanza itakayofanyika ni kufumua
mikataba yote iliyoingiwa bila kufuata taratibu.
Alisema asilimia kubwa ya mikataba iliyoingiwa na Serikali,
haiwanufaishi Watanzania walio wengi na zaidi ya hapo haina tija kwa Taifa.
“Haiwezekani Watanzania wakaishi katika hali ya umaskini wakati
wana rasilimali nzuri, zinazowafanya wafaidi matunda ya nchi yao, lakini kuna
wajanja wachache wanaingia mikataba isiyo na tija, sasa tukiingia madarakani,
tutaifumua,” alisema Profesa Lipumba ambaye leo atakuwa Kijiji cha Msimbati.
Juzi, akiwa katika Mji wa Mikindani mkoani Mtwara aliionya Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuacha kushughulikia suala la Kura ya Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa na badala yake ijikite kuandaa mazingira ya kufanyika
kwa Uchaguzi Mkuu ili kulinusuru Taifa kuingia katika mgogoro usio wa lazima.
Profesa Lipumba alisema NEC isipoteze rasilimali za Taifa na
muda kwa jambo lisilo na tija kwa wakati huu.
“Jaji Lubuva (Damian, Mwenyekiti wa NEC) asiliingize Taifa
katika mgogoro, ana haraka gani na Katiba Inayopendekezwa wakati hili la
uandikishaji katika Daftari la Kudumu la Wapigakura hajalimaliza...?
Ashughulikie hili la daftari ndiyo kazi yake kwa sasa, siyo Katiba,” alisema
Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wananchi.
Chanzo ni
Gazeti la Mwananchi
No comments
Post a Comment