Zinazobamba

Lowassa: Tuliohuzunika, tutashinda pamoja



lowassapx a10b6
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema waliofurahi na kuhuzunika naye pia watashinda pamoja naye.
Bila kufafanua kauli yake jana, Lowassa aliwaambia wakazi wa Monduli mkoani Arusha kuwa: "Kumbukeni kaulimbiu yangu wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja".(HD)
Mbunge huyo wa Monduli alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi mbili za ghorofa za wazazi katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli.
Katika hotuba yake fupi, pia alitamba kwamba atayashinda majaribu. Hata hivyo, hakufafanua majaribu hayo... "Kuna vita kubwa, lakini ambacho naweza kusema ni kuwa nayaweza yote kwa yeye anitiaye nguvu."
Kuhusu afya yake ambayo mara kadhaa imeelezwa kuwa siyo imara, kiongozi huyo alisema kwa sasa ni nzuri na imeimarika kupita kipindi kingine chochote.
Lowassa alisema kuanza ujenzi wa majengo hayo ambayo ni utekelezaji wa ahadi zake, ni moja ya ushindi na kuwataka wakazi wa Monduli, kumshukuru Mungu kwa yanayotokea.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo Nangole aliwataka wakazi wa Monduli, kumshukuru Mungu kwa kuwa na mbunge Lowassa ambaye anapendwa nchi nzima.
"Monduli Mungu awape nini, Lowassa anaitwa kila mahala kusaidia kutokana na moyo wake wa huruma na hapa ametekeleza ilani yote ya uchaguzi," alisema.
Kauli ya Lowassa imekuja siku chache tangu mtangulizi wake katika nafasi ya Waziri Mkuu, Frederick Sumaye alipomtuhumu hadharani kwamba amekuwa akimhujumu na kumwekea vikwazo vya kisiasa kwa kutumia mbinu chafu. Miongoni mwa mambo yaliyoonekana kumkera Sumaye ni habari iliyoandikwa na gazeti hili Septemba 16, mwaka huu inayohusu mradi wa maji Ziwa Victoria, ambayo Lowassa alinukuliwa akisema kuwa wakati akiwa Waziri wa Maji, aliungwa mkono na mawaziri watatu tu alipopendekeza mradi huo wa maji.
Sumaye alisema: "Najua mhusika ametumia sana mradi huu kisiasa na sisi wengine tumenyamaza japo ukweli tunaujua. Amenilazimisha niseme ukweli kuhusu mradi huu kwa sababu mimi nilikuwa Waziri 

Mkuu na mradi umetekelezwa chini ya uangalizi wangu," alisema na kuongeza:
"Kama waziri anaweza kubuni na kutekeleza mradi mkubwa hivyo peke yake, sasa akiwa Waziri Mkuu si maji yangefika Dodoma? Mbona hata bado kuna sehemu za Kanda ya Ziwa bado kuna shida ya maji?"
Tangu Sumaye atoe tuhuma hizo ambazo zinahusishwa na vita ya kuwania urais wa 2015, Lowassa hakuwahi kujibu chochote wala kusikika akizungumza hadharani, hadi jana.Lowassa alisema mafanikio yaliyopatikana katika jimbo lake na mengine nchini, yanatokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambao umefanywa na Rais Jakaya Kikwete.
"Hakuna kipindi ambacho ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa kiasi kikubwa kama kipindi cha Rais Kikwete naomba sote tumpongeze," alisema Lowassa.
Alisema hivi karibuni amekutana na Rais Kikwete ambaye ametoa Sh3 bilioni za ujenzi wa mabwawa 10 katika wilaya hiyo ili kukabiliana na tatizo la maji.
Wodi hizo za kisasa zinajengwa na Kampuni za Meelo Constraction na Bulem Constraction za Arusha kwa gharama ya Sh1.9 bilioni na zitakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 140 wakati mmoja.

Hakuna maoni