WASANII 21 WASAMEHEWA MASHTAKA, SERIKALI YATOA ONYO ZITO KWA MATUMIZI YA MITANDAO
Na Mussa Augustine:Dar es Salaam
Wasanii na watengeneza maudhui 21 wanaotumia mitandao ya kijamii wamefutiwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili, huku Serikali ikiwaonya kutorudia makosa yaliyowahi kuwasababishia matatizo ya kisheria.
Mashtaka hayo yalihusisha makosa mbalimbali, ikiwemo matumizi ya lugha za matusi, kauli zisizo na staha pamoja na vitendo vya kudhalilisha au kutweza utu wa watu wengine.
Akizungumza leo, Septemba 2, 2026, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi, amesema Serikali imeamua kuwafutia mashtaka hao 21 baada ya kubaini kuwa baadhi yao hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kanuni zinazosimamia matumizi ya mitandao ya kijamii.
Waziri Katambi ameeleza kuwa pamoja na kufutiwa mashtaka, wahusika wamepewa maelekezo na miongozo itakayowawezesha kuendelea na shughuli zao kwa kuzingatia sheria.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa msamaha huo haupaswi kuchukuliwa kama ruhusa ya kurudia makosa, akionya kuwa Serikali haitawafumbia macho endapo wataendelea kukiuka sheria na taratibu zinazosimamia matumizi ya mitandao ya kijamii.
“Kila mtu ana haki ya kufanya kazi na shughuli zake kwa mujibu wa sheria, lakini uhuru huo haupaswi kutumiwa kama sababu ya kumvunjia mtu mwingine heshima au kutweza utu wake,” amesema Katambi.
Amesema ni muhimu kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuheshimiana na kufuata sheria na taratibu, akibainisha kuwa kila mtu anapaswa kupata haki zake za msingi bila kujali umaarufu, hadhi au nafasi aliyonayo katika jamii.
“Jambo kubwa ni kuheshimiana na kufuata taratibu. Kila mmoja apewe haki yake ya msingi, awe ana jina au hana jina,” amesema.
Waziri Katambi pia amewahimiza washiriki wa kikao hicho kujenga utamaduni wa kusameheana pale makosa yanapotokea, lakini akaonya kuwa msamaha huo haupaswi kuwa sababu ya mtu kuzoea kurudia makosa yale yale.
“Kutokujua sheria hakumuondolei mtu wajibu pale anapofanya kosa. Hivyo, kila mmoja anapaswa kuhakikisha anafahamu sheria, kanuni na taratibu zinazohusu shughuli anazozifanya,” amesema.
Kikao hicho kilichowakutanisha watengeneza maudhui mtandaoni (content creators) pamoja na wadau wa sheria, kilijadili kwa kiasi kikubwa umuhimu wa kulinda haki za msingi, kuheshimu utu wa binadamu, kufuata sheria na kutumia uhuru wa kujieleza kwa uwajibikaji.
Washiriki pia walikumbushwa kuwa, pamoja na kila mtu kuwa na haki na uhuru wa kujieleza, haki hiyo ina mipaka pale inapoweza kuathiri au kukiuka haki, heshima na utu wa mtu mwingine.
Serikali imesisitiza kuwa watengeneza maudhui na watumiaji wengine wa mitandao ya kijamii wanapaswa kufahamu sheria, kanuni na taratibu zinazohusu matumizi ya mitandao hiyo ili kuepuka kuingia katika migogoro na masuala ya kisheria.

No comments
Post a Comment