Zinazobamba

TPA YALENGA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MIZIGO BANDARINI.

*Yajenga matanki 15 ya mafuta,ili kupunguza muda wa meli kukaa bandarini kutoka siku 21 hadi saba

Na Mussa Augustine.Dar es salaam 

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza kutekeleza miradi mikubwa ya kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, huku ikilenga kupunguza gharama za mizigo na ucheleweshaji wa meli.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa matanki 15 ya kisasa ya kupokea na kusambaza mafuta, ambao unatarajiwa kupunguza muda wa meli kukaa bandarini kutoka siku 21 hadi siku saba.

Hayo yamesemwa Septemba 4, 2026, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi wa TPA, Mhandisi Eric Madinda wakati wa ziara ya viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu waliotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

Aidha amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya mamlaka hiyo kuongeza ufanisi wa huduma za bandari.

Amesema miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Tank Farm, maboresho ya Gati la Malindi pamoja na eneo la Kurasini Logistics Centre, linalotumika kama nyongeza ya bandari katika kuhudumia mizigo.

*Meli kukaa siku saba.

Madinda alisema Tank Farm itakuwa na matanki 15 yatakayotumika kupokea na kusambaza mafuta kwa kampuni za usambazaji wa mafuta (OMCs).

“Mradi huu unalenga kupunguza muda wa meli kukaa gatini kutoka siku 21 za awali hadi siku saba pekee, huku meli ikihudumiwa kwenye gati kwa saa 24 na kukaa nangani kwa siku sita,” amesema.

Amesema kupungua kwa muda huo kutasaidia kupunguza gharama za ucheleweshaji wa meli (demurrage), ambazo awali zilifikia takriban dola 25,000 za Marekani kwa siku.

Kwa mujibu wa Madinda, hatua hiyo hatimaye itasaidia kupunguza gharama za mafuta na kumwezesha mlaji wa mwisho kupata bidhaa hiyo kwa bei nafuu zaidi.

*Gati la meli kubwa.

Madinda alisema TPA pia ina mpango wa kujenga gati jipya eneo la Kendo litakalokuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa hadi nne kwa wakati mmoja, zenye uzito kati ya tani 150,000 na 200,000 (DWT).

Amesema kwa sasa eneo la Single Point Mooring (SPM) linapokea meli zenye uzito wa DWT 100,000, huku Kurasini Oil Jetty (KOJ) likipokea meli za DWT 45,000.

Aidha, amesema kuna mpango wa kuhamisha KOJ na kujenga magati namba 12 hadi 15.

SGR, MGR kupunguza msongamano.

Katika hatua nyingine, Madinda amesema TPA inashirikiana na wadau mbalimbali kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa mizigo, ikiwamo matumizi ya reli za SGR na MGR.

Amesema pia kuna mipango ya kujenga barabara za kulipia (toll roads) kutoka bandarini kuelekea Kibaha na Morogoro, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kupunguza msongamano wa malo

*Wanafunzi wapongeza.

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARISU), Osward Maganya, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Uchukuzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya bandari.

Maganya amesema kuongezwa kwa kina cha bahari kufikia mita 15 kutaiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa zaidi.

Amesema pia kuunganishwa kwa SGR na MGR na bandari hiyo kutasaidia kusafirisha mizigo kwa haraka na kupunguza msongamano wa malori barabarani

Naye Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Kasti Karen Mary, aliishukuru Wizara ya Uchukuzi kwa kuwawezesha wanafunzi kutembelea miradi hiyo na kujifunza kwa vitendo.

Amewataka vijana kutumia fursa zinazopatikana katika sekta ya uchukuzi na bandari kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.



No comments