NIDA YAWATAKA WANANCHI KUCHUKUA VITAMBULISHO VILIVYOKAMILIKA.
DAR ES SALAAM:
Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wananchi waliojisajili na ambao vitambulisho vyao vya taifa vimekamilika kufika katika ofisi za NIDA na kuvichukua, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya Mwezi wa Utambulisho.
Kampeni hiyo imeanza Septemba 1 na inatarajiwa kuendelea hadi Septemba 30, 2026, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kujisajili, kuchukua vitambulisho vyao vya taifa pamoja na kuongeza matumizi sahihi ya utambulisho katika upatikanaji wa huduma mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Greyson Msigwa, amesema kampeni hiyo inafanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani, ambayo huadhimishwa Septemba 16 kila mwaka.
Msigwa amesema maadhimisho hayo nchini yatafanyika katika ofisi za NIDA zilizopo katika wilaya mbalimbali za Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya ya ID for Africa, inayolenga kuhamasisha na kuimarisha mifumo ya utambulisho barani Afrika, hususan kuhakikisha wananchi wanapata utambulisho wa kisheria unaowawezesha kupata huduma na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Katika mwaka 2025, Tanzania ilipata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano mkuu wa ID for Africa, ulioshirikisha takribani nchi 48 kati ya nchi 54 za Afrika.Mkutano huo ulikuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha harakati za utambulisho barani Afrika na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa utambulisho wa kisheria,” amesema Msigwa.
Amesema juhudi hizo zimechochewa na tathmini mbalimbali zinazoonesha kuwa bara la Afrika lina idadi kubwa ya watu wasio na utambulisho wa kisheria, hali ambayo imeifanya nchi za Afrika kuunganisha nguvu kuhakikisha wananchi wanatambuliwa na kupata utambulisho unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
WATU MILIONI 27 WAJISAJILI NIDA
Kwa upande wa Tanzania, Msigwa amesema Serikali ilianza mchakato wa usajili na utambuzi wa watu kwa ajili ya utoaji wa vitambulisho vya taifa baada ya kuweka misingi ya kisheria na kisera ya usajili na utambuzi wa watu nchini.
Amesema hatua hiyo ilifuatiwa na utekelezaji wa Sheria ya Usajili na Utambuzi wa Watu, iliyoweka msingi wa kuanzishwa kwa taasisi maalumu ya kusimamia masuala ya utambulisho.
“Mwaka 2008, Serikali ilianzisha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambayo imepewa jukumu la kusimamia usajili na utambuzi wa watu nchini pamoja na utoaji wa vitambulisho vya taifa,” amesema.
Kwa mujibu wa Msigwa, hadi kufikia Julai 2026, zaidi ya watu milioni 27 walikuwa wamesajiliwa katika mfumo wa NIDA, sawa na zaidi ya asilimia 87 ya watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea nchini.
Ameongeza kuwa zaidi ya vitambulisho milioni 21 vya taifa vilikuwa vimezalishwa, huku idadi kubwa ya wananchi ikiwa tayari imekabidhiwa vitambulisho vyao.
Hata hivyo, amesema bado kuna wananchi ambao wameshasajiliwa na vitambulisho vyao vimekamilika, lakini hawajafika katika ofisi husika kuvichukua.
Kutokana na hali hiyo, NIDA imetumia kampeni ya Mwezi wa Utambulisho kuwakumbusha wananchi waliopata taarifa kuwa vitambulisho vyao vimekamilika kufika katika ofisi husika na kuvichukua.
UTAMBULISHO WA KISHERIA WAWEZESHA UPATIKANAJI WA HUDUMA.
Msigwa amesema maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani yanahusishwa na Lengo la 16.9 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), linalosisitiza umuhimu wa kuhakikisha watu wote wanapata utambulisho wa kisheria.
Amesema utambulisho wa kisheria hauishii katika kuwa na nyaraka au kitambulisho pekee, bali ni msingi unaomwezesha mtu kutambulika kwa usahihi, kupata haki na huduma mbalimbali pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Aidha, amesema mfumo madhubuti wa utambulisho huiwezesha Serikali kuimarisha usalama, kupanga huduma, kusimamia rasilimali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
TAASISI 157 ZUNGANISHWA NA MFUMO WA NIDA.
Katika kuendelea kuimarisha matumizi ya utambulisho, Serikali imekuwa ikitekeleza mfumo wa kuunganisha taasisi mbalimbali na Mfumo wa Usajili na Utambuzi wa Watu unaosimamiwa na NIDA.
Msigwa amesema hadi kufikia Agosti 2026, jumla ya taasisi 157 zilikuwa zimeunganishwa na mfumo huo, zikiwemo taasisi 72 za Serikali na 85 za sekta binafsi.
“Kuunganishwa kwa taasisi hizo kunawezesha uhakiki wa taarifa za watu wanaopata huduma na kusaidia kupunguza matumizi ya taarifa za kughushi,” amesema.
Ameongeza kuwa mfumo huo pia unazisaidia taasisi kujiridhisha kuhusu utambulisho wa watu wanaowahudumia, kuwaajiri au kufanya nao biashara.
Kwa mujibu wa NIDA, matumizi sahihi ya mfumo wa utambulisho yanaweza kusaidia taasisi na wafanyabiashara kupunguza vihatarishi vya kufanya shughuli na watu wenye taarifa zisizo sahihi au utambulisho usiojulikana.
NIDA YATOA ONYO KUHUSU MATUMIZI YA KITAMBULISHO
Katika hatua nyingine, NIDA imewataka wananchi kuhakikisha vitambulisho vya taifa vinatumika na wenyewe pekee na kutovikabidhi kwa watu wengine kwa matumizi yasiyo sahihi.
“Kitambulisho chako ni mali yako. Usimpe mtu mwingine akakitumie kusajili laini ya simu au kufanya shughuli nyingine kwa jina lako,” imeelezwa.
Aidha, mfumo wa utambulisho unasaidia taasisi za ulinzi na usalama katika kudhibiti uhalifu wa kimtandao, utakatishaji wa fedha na vitendo vingine vya kihalifu kupitia uhakiki wa taarifa za watu.
KAULIMBIU: “KIPO, KICHUKUE; KAMILISHA SAFARI YAKO”
Msigwa amesema kaulimbiu ya kampeni ya Mwezi wa Utambulisho nchini ni “Kipo, Kichukue; Kamilisha Safari Yako”, yenye lengo la kuwakumbusha wananchi ambao wamejisajili na ambao vitambulisho vyao vimekamilika kufika na kuvichukua.
Amesema katika kipindi chote cha Septemba, NIDA itaendelea kutoa huduma mbalimbali, zikiwemo usajili wa wananchi wenye sifa, ugawaji wa vitambulisho vya taifa, marekebisho ya taarifa pamoja na utoaji wa elimu kuhusu matumizi sahihi ya utambulisho.
Kampeni hiyo inatarajiwa kuhusisha Serikali, vyombo vya habari, taasisi za umma, sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla.
NIDA imeeleza kuwa safari ya utambulisho haikamiliki kwa mwananchi kusajiliwa na kupewa Namba ya Utambulisho wa Taifa pekee, bali hukamilika pale utambulisho huo unapomwezesha kupata huduma kwa urahisi, usalama na ufanisi.
Wananchi wamehimizwa kutumia fursa ya Mwezi wa Utambulisho kufuatilia taarifa zao, kuchukua vitambulisho vilivyokamilika na kuhakikisha wanatumia utambulisho wao kwa usahihi.

No comments
Post a Comment