JUKWAA LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI 2026 KUFANYIKA DODOMA,WASHIRIKI 3000 KUTOKA NDANI NA NJE YA NCHI KUSHIRIKI
Na Mussa Augustine.
Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) limetangaza rasmi kufanyika kwa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026, litakalofanyika kuanzia Oktoba 20 hadi 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, likiwakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa jukwaa hilo Jasper Makala amesema jukwaa hilo linalandaliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, likilenga kujadili mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Jukwaa hilo la mwaka huu litabeba kaulimbiu isemayo,
“Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Uwazi na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza mashirika hayo kutumia mbinu bunifu katika utekelezaji wa shughuli zake, kuimarisha uwajibikaji pamoja na kuongeza uwezo wa kujitegemea kifedha.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la NaCoNGO Bi.Fransisca Mboya amesema jukwaa hilo litawakutanisha wanachama wa mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari na wadau wengine muhimu kwa lengo la kujadili mustakabali wa sekta hiyo na mchango wake katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, mijadala mbalimbali itafanyika ikijikita katika namna mashirika yasiyo ya kiserikali yanavyoweza kuongeza ufanisi wa utendaji, kuimarisha vyanzo vya ndani vya fedha, kutumia teknolojia na ubunifu pamoja na kuendeleza misingi ya uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha amewataka wadau wote wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo muhimu, likisisitiza kuwa sekta hiyo ina nafasi kubwa katika kusaidia juhudi za serikali za kuboresha maisha ya wananchi kupitia elimu, afya, uchumi na huduma nyingine za kijamii.


No comments
Post a Comment