ZIMAMOTO WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA TARURA,TANESCO.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo DC Albert Msando.
Na Mussa Augustine.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limetakiwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) pamoja na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) katika ujenzi wa barabara na uunganishaji wa umeme ili, pindi majanga ya moto yanapotokea, iwe rahisi kuyadhibiti.
Agizo hilo limetolewa Mei 4, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Zimamoto Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Hakikisheni TARURA wanapojenga barabara mshirikiane nao ili kurahisisha miundombinu ya barabara ipitike kirahisi pindi majanga ya moto yanapotokea,” amesema DC Msando.
Ameongeza kuwa, “Pia TANESCO mshirikiane nao katika uunganishaji wa mifumo ya umeme kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo masoko na maduka, ili kuwa na mifumo imara ya kufikika mara majanga ya moto yanapotokea.”
DC Msando ameongeza kuwa Zimamoto wanatakiwa kujiridhisha ubora wa vifaa vinavyotumika kuunganisha umeme kwenye masoko na maduka, na endapo watabaini vifaa hivyo haviko salama, aliyeunganisha huduma hiyo achukuliwe hatua za kisheria.
Kwa upande wake,Naibu Kamishna wa Zimamoto na Uokoaji Tanzania na msemaji wa jeshi hilo,DCP Puyo Nzalayaimisi, ameishukuru Serikali kwa kulipatia magari na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuzima moto na kufanya uokoaji pindi majanga yanapotokea.
“Tunashukuru sana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliboresha jeshi letu kwa kutupatia vifaa vya kisasa, na sisi tunaendelea kujitoa kwa moyo wa dhati katika kuwahudumia wananchi,” amesema.
SACF Mabusi Peter
Awali, Kamanda wa Jeshi hilo Mkoa wa Kizimamoto Ilala, SACF Mabusi Peter, amesema kuwa sasa wapo kwenye mchakato wa kufungua vituo vingine vinne vya zimamoto katika maeneo ya Kinyerezi, Kivule, Masaki na Kigamboni.
Pia amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kushirikiana vizuri na wadau mbalimbali pamoja na kutoa elimu kwa washirika wa zimamoto, na kwamba kwa sasa lina wadau wa kujitolea wapatao 75, pamoja na klabu 50 zenye wanachama 1,000.





No comments
Post a Comment