Zinazobamba

WAKUFUNZI 25 WA VETA KWENDA FINLAND KUPATA UJUZI SEKTA YA MADINI


Na Mussa Augustine

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema kuwa wizara hiyo inatarajia kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta ya madini kwa kutoa mafunzo mbalimbali yanayolenga kuinua sekta hiyo.

Profesa Mkenda amesema hayo Mei 5, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaaga wakufunzi 25 wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwenda nchini Finland kujifunza ujuzi wa teknolojia zinazohitajika katika uchimbaji na ukuzaji mnyororo wa thamani wa madini.Amesema kuwa wakufunzi hao wanapaswa kutumia vyema fursa hiyo ili kurejea na ujuzi utakaosaidia kukuza shughuli za uchimbaji na kuongeza thamani ya madini nchini.

Prof. Mkenda amesema ujuzi watakaoupata utawawezesha kuimarisha shughuli za madini na kuongeza ushindani wa madini ya Tanzania katika soko la kimataifa.

“Taifa linatarajia kupitia VETA wataalamu wengi zaidi watazalishwa ili kusaidia kuongeza thamani ya madini yetu. Nendeni mkajifunze vizuri teknolojia mpya na mbinu bora zitakazokuwa na tija kwa Watanzania,” amesema.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa mradi huo wa kimkakati unatarajia kuwafikia zaidi ya Watanzania 400, hasa kutoka jamii zinazojihusisha na shughuli za uchimbaji madini, huku kipaumbele kikitolewa kwa wanawake na makundi maalum.

CPA Kasore ameongeza kuwa wakufunzi hao watakaporejea wataeneza ujuzi kwa wenzao pamoja na kuwezesha kuanza kutumika kwa mitaala sita mipya, ikiwemo inayohusu sekta ya madini.Halikadhalika, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dk. Mwajuma Lingwanda, amesema mradi huo utaongeza ubora wa mafunzo ya ufundi stadi katika sekta ya madini na kuleta matokeo chanya kwa taifa.Wakati huo huo, mwakilishi wa Wizara ya Madini, CPA Zephaniah Henry, amesema bado kuna uhaba wa wataalamu wa uchimbaji madini nchini, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuziba pengo hilo na kuongeza wataalamu wenye ujuzi wa kisasa katika sekta ya madini.Akizungumza kwa niaba ya wakufunzi hao, mkufunzi kutoka VETA Dodoma, Neema Lyimo, amesema wamebeba matumaini ya vijana wa Tanzania na wana dhamira ya kuimarisha sekta ya madini kupitia ujuzi watakaoupata nchini Finland.

Wakufunzi hao wanatarajiwa kujifunza masuala mbalimbali, ikiwemo uchimbaji wa kisasa wa madini (digital mining), usalama na afya migodini, utunzaji wa mazingira pamoja na uendeshaji wa mitambo ya kisasa inayotumika katika uchimbaji wa madini.




No comments