NONDO ASEMA VIJANA 78 PEKEE WAMEPATA MIKOPO, SIYO 1,961
Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa ya Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo, ametoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Vijana kufungua dirisha la awamu ya pili la mikopo kwa vijana ili kutoa fursa kwa kundi lingine kuomba mikopo hiyo.
Nondo amesema hayo leo Mei 8,2026 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao makuu ya chama hicho.
Amefafanua kuwa kati ya vijana 30,384 walio omba mikopo katika awamu ya kwanza, vijana 78 pekee ndio waliopata mikopo hiyo.
Ameendelea kufafanua kuwa idadi ya wanufaika 78 aliyoitoa ni tofauti na ile iliyotangazwa na Wizara husika, ambayo imesema vijana 1,961 walipata mikopo kati ya waombaji 30,384.
Amesema idadi ya wanufaika 78 aliyoipata ni ya majina yaliyotajwa kwenye taarifa ya Wizara, huku akieleza kuwa hajui idadi iliyoongezeka hadi kufikia 1,961 imetoka wapi.
Amesema hata yeye aliomba peke yake, lakini katika jedwali ameongezewa majina ya watu 10 ambao hawafahamu wala hawatambui.
“Ni vyema Wizara ya Maendeleo ya Vijana ikatoa ufafanuzi hawa watu walio ongezwa wametoka wapi ili kila kijana afahamu na kuondoa sintofahamu ya ongezeko hilo,” amesema Nondo.
Waziri wa wizara hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu hakupatikana, hivyo jitihada za kumtafuta zinaendelea ili atoe ufafanuzi wa changamoto hiyo.
Nondo amesema kutokana na idadi ndogo ya vijana waliopata mikopo katika awamu ya kwanza, ni vyema dirisha la awamu ya pili lifunguliwe ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kuomba mikopo hiyo.
Hata hivyo, ameshauri kuwa ili kuwezesha vijana wengi kupata mikopo, baadhi ya vigezo viondolewe, ikiwemo kigezo cha leseni ya biashara, kwani baadhi yao wanaomba mikopo hiyo ili waanze kufanya biashara.
Pia ameshauri kuwa fedha zilizopelekwa katika wizara za kisekta zirejeshwe katika Wizara ya Maendeleo ya Vijana ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kupata mikopo tofauti na ilivyo sasa.
Aidha, ameiomba wizara hiyo kueleza kwa kina sababu zilizowafanya baadhi ya vijana kukosa mikopo hiyo ili waweze kufanya marekebisho katika awamu ya pili ya uombaji wa mikopo, hatua ambayo itasaidia vijana wengi zaidi kunufaika.

No comments
Post a Comment