NCCR Mageuzi Yawaonya Wanaotoa Kauli za Kejeli Kuhusu Uteuzi wa Dkt. Munis
Chama cha NCCR Mageuzi kimetoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao wamekuwa wakimshambulia kwa maneno Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Aveline Munis, baada ya kuteuliwa na Rais Dkt. Samia kuwa Mbunge na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano.
Onyo hilo limetolewa Mei 7, 2026 na Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa chama hicho, Faustine Sungura, wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama jijini Dar es Salaam.
Amesema viongozi hao wamekuwa wakidai kuwa Dkt. Munis si mwanachama halali wa chama hicho na kwamba hakupaswa kuteuliwa katika nafasi hiyo.
Aidha, amesema baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakieneza chuki hizo kwa maslahi yao binafsi na kwamba jamii inapaswa kuwapuuza viongozi hao, huku chama hicho kikipanga kuwachukulia hatua kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
Pia amesema kuwa chama hicho kitampa ushirikiano, heshima na mazingira mazuri ya kazi Dkt. Aveline Munis ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kipindi chote cha uongozi wake.
Vilevile, chama hicho kimemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukipa heshima kwa kumteua Katibu Mkuu wa chama hicho kushika nafasi ya uongozi ndani ya Serikali.
Sungura amesisitiza kuwa chama hicho kimepokea uteuzi huo kwa mikono miwili na kina imani na uwezo wa Dkt. Munis katika kuitumikia Serikali pamoja na wananchi.
“Baadhi ya watu wasiokitakia mema chama chetu wamekuwa wakitumia nafasi zao kumshambulia na kumkejeli Dkt. Munis kwa lengo la kumkatisha tamaa, lakini chama hakitaruhusu hali hiyo kuathiri utendaji wake,” amesema Sungura.
Ameongeza kuwa, “NCCR Mageuzi itampatia ushirikiano Dkt. Aveline Munis katika kutetea jimbo lake na kusimamia maslahi ya chama pamoja na Taifa kwa ujumla.”
Aidha, amesema chama hicho kinajivunia kuona mwanachama wake amepewa nafasi ya Naibu Waziri, akieleza kuwa hatua hiyo ni ishara ya kuaminiwa kwa chama hicho na viongozi wake.

No comments
Post a Comment