Zinazobamba

BODI YA MADALALI YAZINDULIWA

*Lengo ni kudhibiti madalali matapeli.

Na Mussa Augustine.

Kampuni ya Mkuyu Africa Builders and Developers Real Estate imezindua bodi ya madalali nchini, “Tanzania Brokers Association Board” (TBAB) itakayosimamia haki na shughuli zote zinazofanywa na madalali kwa mujibu wa sheria.

Hatua hiyo ni muhimu kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la madalali wasio waaminifu ambao hufanya kazi zao kinyume cha sheria hali ambayo inaichafua tasnia hiyo katika jamii.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mkuyu Africa Builders and Developers Real Estate,Judeid Othman amesema kwamba kampuni yake imeanza kuchukua hatua ya kupigania haki za madalali tangu mwaka 2016 ndipo ilipoamua kuanzisha bodi hiyo ili kuwezesha madalali kujisajili na kutambulika kisheria.

“Bodi hii ya Madalali itasaidia kuwarasmisha madalali,kuweka uwazi na uwajibikaji,kuwafanya waaminike katika jamii,na kulinda maslahi ya wateja na madalali wakati wa kufanya mauziano ya mali zisizohamishika kama vile uuzaji wa nyumba na viwanja,” amesema Othman.

Ameongeza kuwa ana furaha kuwaambia madalali kuwa kazi yao inahitaji uaminifu wa hali ya juu kwa wateja wao, hivyo wajisajili kwenye bodi hiyo ili taarifa zao zipatikane kwa urahisi hali itakayosaidia wateja kupata huduma zao kwa wakati na weledi mkubwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Emmanuel Machibya amesema kwamba kazi ya udalali ni kazi ambayo inaheshimika na kwamba endapo dalali akiiheshimu inamfanya awe na maisha bora kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta nyingine.

Aidha, amesema kuwa bodi hiyo itahakikisha inawasimamia madalali wote kwa kuzingatia sheria na kwamba sasa ni wakati wa wao kuheshimika katika jamii.

“Kwa sasa mtu akisema yeye ni dalali, asilimia kubwa ya jamii inamuona ni tapeli, lakini kwa mataifa ya Ulaya kumuona dalali ni jambo gumu sana kwa sababu wanaheshimika sana, sasa tunataka na Tanzania madalali waheshimike, kazi ya udalali inaendana sambamba na kazi ya uanasheria,” amesema Machibya ambaye kitaaluma ni mwanasheria.

Naye Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Bi Leonida Ibrahim ambaye ni dalali wa muda mrefu, amewakumbusha madalali wenzake kuwekeza kwenye miradi mbalimbali pindi wanapopata pesa kwenye kazi zao.

“Madalali wanapata pesa nyingi sana, lakini wengi wao wanazitumia hovyo, nawasihi kukumbuka kuwekeza ili waweze kuzalisha kwa maisha ya baadaye,” amesema Leonida.

Hata hivyo, baadhi ya washiriki wa hafla hiyo ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wamepongeza hatua hiyo na kubainisha kuwa itasaidia kuwaheshimisha wale wote watakaoamua kuwa madalali na kujisajili kwenye bodi hiyo.




No comments