Zinazobamba

SALAMU ZA PONGEZI KWA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE KUFUATIA UTEUZI HUU AFRIKA:

CUF- Chama Cha Wananchi kimepokea kwa furaha kubwa taarifa ya kuteuliwa kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne (4) Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) katika eneo la Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.

Uteuzi huo uliofanywa na Mwenyekiti wa AUC Mhe. Mahmoud Ali Youssouf ni Heshima kubwa kwa Taifa na kwa Mhe. Jakaya Kikwete. Kwetu sisi CUF- Chama Cha Wananchi, Mhe. Kikwete anabaki kuwa Kiongozi pekee aliyejaribu kuruhusu Demokrasia ya Vyama vingi ichukue nafasi nchini japo kwa kiwango cha wastani.

Ni katika kipindi chake cha Uongozi pekee ndipo kura ya mtanzania iliheshimiwa japo kwa 30% hususan katika Chaguzi za Ubunge, Udiwani na Serikali za mitaa.

Msimamo wake wa kukubali kukosolewa na kuamini kwake kwamba hoja kinzani hujibiwa kwa hoja badala ya kumfanya adui aliyetoa hoja, kulipelekea Mhimili wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ufikie kiwango chake cha juu kabisa cha Ufanisi na kupelekea 'madudu' yaliyofanywa na Serikali katika Awamu hiyo na Awamu zilizoitangulia kujadiliwa kwa uwazi na kufikia Maamuzi kwa Maslahi mapana ya Tanzania. 

Haikuwa ajabu kuona kwamba ni katika Awamu yake ya Uongozi ndipo angalau dhamira ya kuipatia Tanzania Katiba Mpya inayotokana na Maoni ya Wananchi ilidhihirika kwa kuasisi Mchakato ambao kwa bahati mbaya haukufikia mwisho.

Ni kutokana na rekodi hiyo muhimu wakati wa Uongozi wake kama Rais ndio sisi CUF- Chama Cha Wananchi tunaamini kwamba Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ataitendea haki nafasi hii aliyopewa. 

Tunamtakia Utendaji uliotukuka katika nafasi hii ndani ya AUC huku tukimkumbusha kwamba ana dhima pia katika kuhakikisha kwamba Utawala Bora na Demokrasia ya Kweli vinarudi na kuimarika Tanzania, akiwa kama Mshauri wa Karibu wa Utawala uliopo.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa 

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge, Sera na Utafiti na Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma 

CUF- Chama Cha Wananchi 

Machi 26, 2026```

No comments