Zinazobamba

WATU 46 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA WIZI

Na Mussa Augustine.

Jeshi la Polisi kanda Maalumu ya Dar es salaam limewatia mbaroni  watu wapatao 46 kwa tuhuma za makosa ya kijinai ikiwemo,nyang'anyi wa kwa kutumia nguvu, kuvunjaji wa nyumba na maghala(Godown)pamoja na wizi mali mbalimbali.

Akizungumza leo Februari 24,206 na Waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam SACP Jumanne Muliro amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika kipindi cha kuanzia Januari 30 hadi Februari 24, 2026.

Kamanda Muliro amebainisha   kuwa baadhi ya watuhumiwa hao walikuwa wakitumia pikipiki na silaha za jadi kama vile mapanga kutekeleza uhalifu huo,hususan maeneo ya pembezoni mwa jiji la Dar es salaam.

Aidha sambamba na hilo amesema kuwa wapo watuhumiwa waliokuwa wakijihusisha na kuvunja nyumba mchana na usiku na kuiba vifaa mbalimbali,huku wengine wakihusika na kununua na kuuza mali za wizi.
"Jeshi la polisi limekamata pikipiki zaidi ya 20(Vishandu),simu 110,runinga,redio na vifaa vingine vya kielektroniki,pia zimekamatwa funguo maalum zenye uwezo wa kufungua kufuli aina mbalimbali pamoja na gari aina ya Toyota Noah yenye namba ya usajili T.457 CQF iliyokuwa ikitumika kusafirisha mali za wizi" amesema SACP Muliro.

Aidha Kamanda Muliro amewataja washukiwa hao kuwa ni pamoja na Rashidi Mtunguja maarufu “Msamba” na wenzake wanne ambao walikamatwa maeneo ya Jangwani,huku Issa Nasoro Kurukutu na wenzake wawili walikamatwa maeneo ya  GongolaMboto,pamoja na Nicholas Abdallah Said mkazi wa Manzese.

Katika hatua nyingine SACP Muliro amesema kuwa  jeshi hilo linaendelea na  ufuatiliaji ili kuwakamata wahusika wote kabla au baada ya kutekeleza uhalifu,sambamba na kuzingatia misingi ya kisheria ikiwemo kukusanya ushahidi, kuwafikisha watuhumiwa Ofisi ya Mashtaka na hatimaye mahakamani. 

Hata hivyo amebainisha kuwa hatua za kisheria zilizochukuliwa ni pamoja na baadhi ya watuhumiwa kuhukumiwa vifungo vikali ikiwemo kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ubakaji wa kundi na unyang’anyi wa kutumia silaha.

"Miongoni mwao ni Mwita Marwa na wenzake wawili waliopatikana na hatia Mahakama ya Kigamboni, Adam Samiro aliyehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, pamoja na Jafari wa Chang’ombe na Omari Omari wa Mbande waliopata adhabu kali Mahakama ya Temeke."amesema Muliro 
Akizungumzia kuhusu usalama barabarani,SACP Muliro amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria,hususani wanaopita kwenye barabara za mwendo kasi.

Aidha amesema kuwa Jumla ya madereva 250 walikamatwa katika kipindi hicho,wakiwemo bodaboda 167, bajaji 19 na magari 64,hatua iliyolenga kupunguza ajali na kero kwa watumiaji wa barabara. 

"Jeshi la Polisi linawasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu,na tunaahidi kuendelea kulinda usalama ili shughuli za kiuchumi,kijamii na kisiasa ziendelee kufanyika kwa amani." amesema. 

No comments