Zinazobamba

BARAZA KUU LA UONGOZI CUF TAIFA LAMCHAGUA ENG. HAMAD MASOUD HAMAD KUWA KATIBU MKUU:

Mwenyekiti Mpya wa CUF- Chama Cha Wananchi Mhe. Yusuf Mirambo Camil amekiongoza Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) kwenye Ukumbi wa Shaaban Khamis Mloo akiambatana na Makamu Mwenyekiti Zanzibar Mhe. Haroub Mohamed Shamis na Makamu Mwenyekiti Bara Mhe. Miraji Mtimbwiriko, waliochaguliwa jana kwenye Ukumbi wa Lekam Social Hall, Buguruni.

Kikao cha BKUT pamoja na mambo mengine kimemchagua Eng. Hamad Masoud Hamad kuwa Katibu Mkuu wa Chama. Aidha, Kikao cha BKUT kimewathibitisha Mhe. Zainab Amiri Mndolwa kuwa Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi; Mhe. Mohamed Zuberi Kirungi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Itifaki na Udhibiti na Eng. Mohamed Mshamu Ngulangwa kuwa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge, Sera na Utafiti.

Pamoja na majukumu hayo, Eng. Mohamed Ngulangwa pia atakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma. 

Awali Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilithibitisha Uteuzi wa Mhe. Eng. Hamad Masoud Hamad na Mhe. Rukia Kassim kuwa wajumbe wa BKUT.

Akitoa hotuba yake ya kwanza Mwenyekiti alisisitiza  umuhimu wa Umoja na Mshikamano na kuwa tayari kusahau mabaya yote yaliyopita ili kuhakikisha Chama kinaimarika na kuweza kufikia Malengo yake ya kushika Dola.

HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!

Eng. Mohamed Ngulangwa 

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge, Sera na Utafiti na Kaimu Mkurugenzi wa Habari 

CUF- Chama Cha Wananchi 

Februari 22, 2026```

No comments