Zinazobamba

Mbeto : CCM si chama cha kibaguzi,kila Mwanachama ruksa kuwania Uongozi

Na Mwandishi  wetu, Zanziabr 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema sera zake  tokea enzi za ASP na TANU,  si za kibaguzi kwa namna  yoyote aidha iwe ni kutokana na  rangi, kabila,asili au nasababu  za watu. 

Vile vile kimesisitiza  kina  wanachama wenye  asili zote wakiwemo Wahindi ,Waafrika, Waarabu, Wachina, Washirazi na Wangazija ambao  kila mmoja ana haki sawa ndani ya CCM   .

Katibu  wa Kamati Maalum  ya NEC Zanzibar  Idara  ya itikadi,Uenezi na Mafunzo ,Khamis  Mbeto  Khamis,  ameeleza hayo huku akiwahimiza  watendaji ,wagombea  au  mwanachama,  atakaetumia maneno  ya kibaguzi, chama hakitamvumilia .

Mbeto alisema  chama cha ASP  visiwani Zanzibar  hakikungwa mkono na Waafrika peke  yao bali  makundi  yote ya kijamii bila kujali asili na rangi zao , walikipigia kura kuanzia uchaguzi wa mwanzo  mwaka 1957 hadi sasa.

Alisema  Mwanachama yeyote akiwa Baniani, Kumbaru, Mwarabu anayetokea  Oman au Yemen, Mshiraz wa Iran  au Muafrika toka  Tanganyika, Kenya ,Malawi ,  Uganda  , Zanzibar au  Comoro wote ni wana CCM. 

'Hatuwezi kwenda kinyume na sera zetu za msingi. Moja kati ya imani yetu  ni kuamini kuwa binadamu wote ni sawa na  Afrika ni moja.Ndio maana CCM  kina viongozi  , Wawakilishi ,Wabunge na wanachama wa rangi na kabila zote" Alisema Mbeto 

Aidha  ,alisema  mwanachama atakaebainika  anatumia lugha ya  ukabila, rangi na kufanya  upendeleo  katika uchaguzi  wa chama, ataadhibiwa kwa mujibu wa katiba  ya CCM ,kinidhamu na kimaadili. 

'Vyama vyenye  sera  za Ubaguzi  wa rangi, asili na nasaba vinafahamika na viongozi wake  hujifaharisha kwa kutoa  matamshi ya  ubaguzi .Siasa hizo ndani  ya CCM  hazina nafasi "Alieleza 

Katibu huyo Mwenezi  aliongeza kusema  vyama  vyenye sera za Ukanda, Udini na ukabila, haviwezi kuungwa mkono na watanzania   wenyewe huku vyama  hivyo  vikikaribia kufa baada ya Watanzania kuvistukia.

Mbeto  amezielekeza Kamati zote za uchaguzi  kuanzia  ngazi za Matawi,Wadi, Majimbo ,Wilaya hadi Mikoa,  zitimize wajibu wa kikatiba na kikanuni kwa  kusimamia  haki na maadili .

"CCM kimeziandikia Taasisi za Serikali zinazohusika na masuala ya  rushwa ikiziomba zifuatilie chaguzi zake  zote. Mwanachama , mgombea au kiongozi atakayekamatwa akitoa au kupokea rushwa  atafikishwa mahakamani" Alieleza.

Hakuna maoni