Zinazobamba

TAWIDO YAIOMBA SERIKALI KUTENGA BAJETI YA VITENDO VYA UKATILI

                      Sophia Lugilahe

Na Mussa Augustine. 

Serikali imeombwa kutenga bajeti ya kushughulikia vitendo vya kikatili ili kutoa nafasi kwa watumishi wa ustawi wa Jamii kuwa na fungu la kufutilia vitendo hivyo.

Wito huo umetolewa leo Agost 21,2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika  lisilo la kiserikali linalopinga  ukatili wa kijinsia kwa wanawake, wanaume na watoto (TAWIDO) Sophia Lugilahe wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake.

Bi Lugilahe amesema kuwa Wakati mwingine watumishi wa ustawi wa Jamii wanapopewa taarifa za vitendo vya kikatili wanashindwa kufuatilia kwa wakati kutokana na kutokuwa na fedha,hali ambayo inasababisha kuzorotesha harakati za kudhibiti vitendo vya ukatili  kwa Jamii.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo wa TAWIDO ametoa wito kwa   Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya Marekebisho ya Sheria ili kudhibiti vitendo vya ukatili vinavyoendelea kushamili kwenye jamii.

Halikadhalika ameomba  Mahakama  kumaliza kesi za ukatili kwa haraka na kutenda haki kwa watakaokutwa na hatia, hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao ili iwe fundisho kwa wengine wanaotenda makosa kama hayo.

"Jamii kwa ujumla inatakiwa kuungana ili kufichua vitendo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria watuhumiwa wanaojihusisha na vitendo vya Ukatili"amesema

Nakuongeza kuwa "Bunge,Mahakama,Viongozi wa Dini, Waandishi wa habari,Waendesha Bajaji na Bodaboda pamoja na Jamii kwa ujumla tushirikiane kwa pamoja kuchukua hatua kila sekta kwa nafasi yake naamini tutafanikiwa kudhibiti vitendo 

Aidha amewakumbusha  wazazi kuacha  kukwepa majukumu ya kulea watoto wao kwa maana ujenzi wa tabia  njema inaanza kujengwa kwenye malezi na kuwapa ulinzi.

Amesema kuwa katika ofisi ya TAWIDO kuna kituo cha kupokea taarifa za kikatili kupitia simu (Call centre) ambapo tangu mwaka 2021 hadi  mwaka huu wameweza kupokea taarifa za vitendo vya ukatili takribani 38, 238.

Katika takwimu hizo, wanawake ni 27,828 wanaume 9352 na watoto ni 9038 na kuweka wazi taarifa hizo ni kwa wale wanofahamu namba ya kituoni hapo.

Amesema kuwa takwimu hizo zinaonesha jamii haiko salama Jambo ambalo litasababisha  kutokuwepo kwa maendeleo kutokana na uwezo wa kundi la watoto waliolawitiwa ama kubakwa , hivyo hatua za haraka zinatakiwa kuchukuliwa kudhibiti hayo.

Pia amesema katika kipindi hicho ukatili wa kimwili zilikuwa na matukio 12,243 huku ukatili wa kijinsia ukiwa 7403, wa kingono ukiwa 13,216 wa kiuchumi ukiwa 3,375 na watoto ni 938.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva wa Bodaboda na Bajaji Mbezi Beach Tumainieli Elisha amewataka maafisa usafirishaji hao kuhakikisha wanatoa taarifa pindi wanapoona kuna viashiria vya vitendo vya ukatili kwenye maeneo yao ya kazi.

"Tuwe na tabia ya kutoa elimu kwa abiria wetu watende mema, tukifanya hivyo kwa ushirikiano tutafanikiwa, hata vitendo vinavyofanywa na wafanyakazi wa ndani wakati mwingine vinachochewa waajiri wao,tabia ya kuwacheleweshea mishahara,kuwabagua hata wakati wa chakula nahuku wao ndio walinzi wakubwa wa familia wakati tukiwa kazini,hivyo wanafikia hatua wanachukua uamzi mgumu hata wa kuwadhulu watoto nyumbani"amesema Elisha.

Tanzania Women Initiative for development organization ( TAWIDO)S ni Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, wasichana na watoto pamoja na kuwaunganisha kwenye huduma, kutoa elimu za ujasiriamali na kuwaunganisha na fursa zilizopo ili kujiimarisha  kijamii, kisiasa na kiuchumi.


Hakuna maoni