Zinazobamba

WADAU WA HABARI WASEMA UTAWALA JPM NI HATARI KWA WAANDISHI WA HABARI,SOMA HAPO KUJUA

Kajubi Mukajanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT). Picha ndogo Alexander Mnyeti aliyewahi kumweka mahabusu mwandishi
BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limepaza sauti na kusema kuwa katika kipindi cha miaka miwili cha utawala wa Rais John Magufuli kumekuwa na  hofu kwa waandishi wa habari na tasnia nzima imeongezeka na kusababisha wanataalum hao kutofanya kazi kwa uhuru na kwa weledi, anaandika Faki Sosi.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusu siku ya Kimataifa ya Kupinga Jinai Dhidi ya Wanahabari ambayo inaadhimishwa duniani kote.
MCT imesema katika kipindi hicho kumekuwapo na matumizi mabaya ya madaraka, upindishwaji wa sheria, unyanyasaji na hata matamsihi ya vitishio kutoka kwa viongozi wa serikali dhidi ya wanahabari na vyombo vyao.
Amesema katika kipindi hicho wanahabari mbalimbali wamenyanyaswa pamoja na magazeti sita kufungiwa na serikali kufanya uzalishaji kwa madai kwamba yaliandika habari za uchochezi ambazo hazitakiwa na watawala.
Mukajanga amesema kuanzia sasa MCT itaanza kuwafikisha mahakamani watu wote wanawazuia, kuwanyanyasa na kuwapiga wanahabari wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Amesema lengo la MCT na washirika wake ni kuhakikisha inamshtaki mtu mmoja mmoja iliawajibke kwa matumizi mabaya ya madaraka au kwa unyanyasaji.
Ameongeza kuwa MCT inaamini mahakamani ndiyo mahala ambapo haki inatendeka na kwamba linahimiza vyombo vya habari na wananchi kuunga mkono juhudi zake na wadau wengine wa habari kushinikiza ili zifutwe sheria kandamizi zinazofifisha uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari na haki ya kupata taarifa.
Amewakumbusha viongozi wa vyombo vya habari hususani wamiliki, watendaji wakuu na wahariri kuhakikisha wanawalinda waandishi na kuzingatia usalama wao.