Zinazobamba

WANANCHI WA TARIME WAKINUKISHA KWENYE MGODI WA NORTH MARA,SOMA HAPO KUJUA


Siku  chache baada ya Rais Dk. John Magufuli  kukabidhiwa ripoti ya pili ya kuchunguza mchanga wa dhahabu wa Kampuni ya Madini ya Acacia, wananchi wa Tarime wamevamia mgodi wa North Mara kwa siku mbili mfululizo.

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni mwendelezo wa kupinga uonevu unaofanywa na wawekezaji hao kupitia Kampuni ya Acacia.

Taarifa kutoka wilayani Tarime zinadai  kuwa wananchi hao walivamia mgodi huo juzi saa 2.00 usiku na jana asubuhi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao walikwenda hadi kwenye mtambo wa kufua dhahabu na   kufanya uharibifu   huo kabla ya kudhibitiwa na jeshi la polisi.

Hata hivyo shuhuda huyo ambaye hakutaka kutaja jina , alisema vurugu hizo zimetokana na uongozi wa Kampuni ya Acacia kushindwa kuwalipa fidia wananchi waliokuwa na maeneo yao tangu  awali.

Alisema wakati madini yalipogundulika,   wananchi walioondolewa walitathiminiwa mali zao yakiwamo mashamba, nyumba na kuahidiwa kulipwa fidia akini hadi sasa hawajalipwa stahiki zao.

Alisema kwa siku mbili mfululizo  wanachi wenye madai yao walifika katika ofisi za kampuni  na kuona baadhi ya majina ya wanaotakiwa kulipwa fidia yakiwa yamebandikwa katika ubao wa matangazo lakini majina ya wengine yakiwa hayajabandikwa.

“Wale ambao hawakuona majina yao walichukuana na kuvamia   mtambo  wa kufua madini na kuondoka na mawe  ambayo tunahisi mengine yana dhahabu.

“Lakini polisi walifika na kuwatawanya na  mabomu ya machozi,’’kilisema chanzo cha habari hiyo.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga,   alisema alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ingawa aliahidi kuzungumza na waandishi wa habari leo.

“Nimesema hivi, siwezi kuzungumza lolote, sina cha kuzungumza na siwezi kuzungumza na mwandishi hadi hapo tutakapokaa kikao kesho (leo) ndiyo nitasema,’’alisema Luoga.

Alipotafutwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema)   kujua kama hatua ya wananchi hao inatokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi karibuni kuwa atawaongoza wananchi   kuwaondoa Acacia kwa kuwa wamekuwa wakiwaibia kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya Tume ya Rais Magufuli, alisema kwa sasa yupo  Dodoma kwa ajili ya vikao vya Bunge .

Alisema  anachojua ni kuwa wananchi hao wamekuwa wakidai malipo yao kwa muda mrefu.

“Wananchi wamekuwa na malalamiko wakidai malipo yao na tayari mgodi umeshaleta madhara mengi, hilo naweza kusema lakini mengine zaidi ya hayo siwezi kuyajua,’’ alisema Heche