Tigo, RITA kuanza awamu ya nne usajili wa watoto Geita, Shinyanga
Na Mwandishi wetu.
Kampuni
ya simu za mkononi ya Tigo kwa kushirikiana na Wakala wa Usajili,
Udhamini na Ufilisi (RITA)pamoja na UNICEF inategemea kuzindua awamu ya
nne ya usajili wa watoto chini ya miaka mitano katika mikoa ya Geita na
Shinyanga mapema wiki ijayo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na RITA, Mpango huu wa Usajili na kutoa
vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano unatarajiwa
kutekelezwa katika wilaya zote tatu (3) zilizo na halmashauri 6 za mkoa
wa Shinyanga na Wilaya zote tano (5) zilizo na halmashauri sita (6)
katika mkoa wa Geita.
“Kwa
mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, ni asilimia
9.4 ya watoto wa mkoa wa Shinyanga na asilimia 8.6 katika mkoa wa Geita
wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Lengo la RITA mara
itakapoanza kutekeleza mpango huu ni kusajili watoto wote 740,912 ambao
hawajasajiliwa na hawana vyeti vya kuzaliwa katika mikoa yote miwili kwa
kipindi cha miezi 6,” alisemakaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Rita Emmy
Hudson.
Ili
kufanikisha utekelezaji mpango huu kutakuwa na vituo vya usajili zaidi
ya 650 vitakavyokuwa na wasajili wasaidizi wapatao 1,250 kwa mikoa yote
miwili. Wasajili hawa watawekwa katika ofisi za afisa mtendaji wa mtaa
na vile vile katika maeneo ambayo kinamama huenda kupata huduma za
kiafya za watoto.
“Matokeo
tuliyoyapata mwaka jana katika utekelezaji wa mpango huu katika mikoa
ya Iringa na Njombe yatatumika kuhakikisha watoto wote wanapata huduma
hii katika mikoa ya Geita na Shinyanga,” alisema Hudson huku akiongeza
kwamba mikoa hiyo iliweza kusajili watoto kwa asilimia mia moja (100%)
kwa kipindi cha miezi mitano huko Iringa na Njombe.
Meneja
wa Huduma za Jamii wa kampuni ya Tigo, Halima Okash alisema kampuni ya
Tigo imekuwa mshirika mkuu wa mkakati wa Usajili wa Watoto wa chini ya
miaka mitano toka mwaka 2012 ili kuiwezesha serikali kupunguza tatizo la
muda mrefu la watoto kutosajiliwa na mamlaka husika pindi wanapozaliwa
hivyo kuathiri mipango ya maendeleo ya muda mfupi na ile ya muda mrefu.
“Duniani
kote takwimu sahihi na zinazopatikana kwa wakati ni jambo muhimu ili
kufanikisha mipango mbalimbali ya maendeleo ndio maana kati ya malengo
makuu ya mkakati huu ni kutumia teknolojia ya simu za kiganjani katika
kuchukua na kutuma taarika kwenda katika kanzidata (database) ya RITA
mara mtoto anaposajiliwa kwenye vituo vilivyoaainishwa,” alisema Okash.
Okash
aliongeza kwamba kampuni ya simu za mkononi ya Tigo inajivunia kuweza
kutumia rasilimali ya ujuzi tulio nao katika kuwezesha kila mtoto
nayezaliwa kutambuliwa na mamlaka husika hivyo serikali kufahamu kuna
watoto kiasi gani katika umri fulani.
Cheti
cha kuzaliwa ni nyaraka ya awali ya utambulisho kwa mtoto inayomwezesha
kutambuliwa uwepo wake na ni haki ya mtoto ya msingi. Hudson aliwaomba
wadau wote ikiwa pamoja na viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri,
tarafa, kata, mitaa/vijiji na vitongoji kushirikiana kwa pamoja ili
kuweza kufanikisha utekelezaji wa mpango huu.
“Vilevile,tunawaomba
Viongozi wa dini, wanasiasa, wanahabari na viongozi wa jadi ambao
watusaidia kuelimisha wananchi kuhusu kujitokeza kwa wingi kuwasajili
watoto ili wapate vyeti vya kuzaliwa,” alisema Hudson.