BIFU LA MIPAKA KATI YA TANZANIA NA MALAWI YAIBUA SERIKALI YA MAGUFULI,YAIBUKA NA KUSEMA HAYA,SOMA HAPO KUJUA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UFAFANUZI WA
TAARIFA ZILIZOANDIKWA NA BAADHI YA MAGAZETI JUU YA MGOGORO WA TANZANIA NA
MALAWI KWENYE ZIWA NYASA
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika
Mashariki inapenda kufafanua na kuweka sawa taarifa zilizoandikwa kwenye baadhi
ya Magazeti ya tarehe 07 Desemba, 2016 kuwa mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania
na Malawi kwenye Ziwa Nyasa unakaribia kuiva na kwamba Mgogoro huo unatarajiwa
kumalizwa na washauri wa kimataifa.
Taarifa hiyo haikuwa sahihi. Ukweli ni kuwa, mgogoro
wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwa sasa upo chini ya Jopo la Viongozi
Wastaafu wa Afrika wanaotokea kwenye nchi za Ukanda wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Jopo hilo linaongozwa na Mhe. Joachim
Chissano, Rais Mstaafu wa Msumbiji akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais
Mstaafu wa Botswana na Mhe. Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini.
Aidha, Jopo hili ambalo liliundwa na Umoja wa Afrika
kupitia Jukwaa la Viongozi Wastaafu wa Afrika (Forum for Former African Heads
of State and Government) kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro huu, linaendelea na
kazi hiyo kwa kupitia taarifa mbalimbali na maandiko yaliyowasilishwa kwao na
Tanzania na Malawi. Vile vile, Jopo lilikwisha zikutanisha pande zote mbili katika
mashauriano ya awali yaliyofanyika nchini Msumbiji
Wizara inapenda kuujulisha umma kuwa licha ya kuwepo
kwa mgogoro wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika Ziwa Nyasa, mahusiano ya nchi
hizi mbili yamezidi kuimarika siku hadi siku katika Nyanja zote za kiuchumi,
kisiasa na kijamii. Hata wananchi wa pande zote mbili za Ziwa wameendelea
kuishi kwa amani na ushirikiano wa karibu.
Aidha, katika kuimarisha uhusiano huu, Tanzania na
Malawi zinatarajia kuwa na mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano mapema
mwakani. Mkutano huu utawaleta watalaam wa nchi hizi mbili kutoka Sekta
mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto za ushirikiano katika sekta hizo,
kubaini maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuweka mikakati ya kutekeleza
miradi ya pamoja itakayokubaliwa baina ya pande hizi mbili.
Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo unatarajiwa
kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji,
usafirishaji, fedha, nishati, utalii, ulinzi na usalama uhamiaji, uvuvi na
ardhi.
Hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki inawaomba Waandishi wa Habari, Wadau mbalimbali na wananchi
kwa ujumla inapohitajika kupata taarifa sahihi za suala hili kwenda kwenye
Mamlaka husika na kuziandika kwa usahihi kwa ustawi wa nchi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 07 Desemba, 2016.