MAADHIMISHO YA SIKU YA TAKWIMU AFRIKA KUFANYIKA KESHO
WAZIRI wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt.
Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuwa mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya
Takwimu Afrika yatakayofanyika kesho jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa
Makumbusho ya Taifa mkabala na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es
Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa Bw. Daniel Masolwa
kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema dhumuni la kuadhimisha siku hiyo ni
kuongeza uelewa mpana kwa watumiaji wote wa Takwimu Afrika kuhusu umuhimu
wa takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo katika sekta zote za kijamii na
kiuchumi.
“Siku hii huadhimishwa ili kutoa
fursa ya kutathmini na kufuatilia malengo yaliyofikiwa katika Mipango ya
Maendeleo ya ndani na nje ya Nchi”, amesema Masolwa.
Masolwa ameeleza kuwa kaulimbiu ya
maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Kuimarisha Takwimu za Kiuchumi kwa
Mtangamano wa Kikanda, Mabadiliko ya Miundo na Maendeleo Endelevu".
Amefafanua kuwa kaulimbiu ya mwaka
huu inalenga kuwaelekeza wadau mbalimbali wa takwimu kujikita katika kujadili
na kuweka mikakati inayoendana na umuhimu wa kuboresha na kuimarisha takwimu za
uchumi na zenye ubora kwa Utangamano wa Kikanda Barani Afrika.
Maadhimisho ya Siku ya Takwimu
Afrika hufanyika kila mwaka tarehe 18 Novemba ambapo huandaliwa na kaulimbiu
mbalimbali zinazohusiana na umuhimu wa takwimu katika kupanga maendeleo na
kutunga sera katika Bara la Afrika.
MWISHO.
MAELEZO
YA PICHA
Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa
Daniel Masolwa (kushoto) kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea maadhimisho ya Siku ya Takwimu
Afrika yatakayofanyika Novemba 18 katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini
Dar es Salaam, kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Beatrice Lyimo.
Picha na Eliphace Marwa -Maelezo