Zinazobamba

UFISADI WA KUTISHA BANDARINI,MABILIONI PESA YAIBWA,FILIKUNJOMBE AANGUA KILIO NI YALE YALIYOWAI KUIBULIWA NA GAZETI LA JAMHULI,SOMA HAPA KUJUA

                 
Na Narsa Abdallah
KAMATI ya Kudumu ya Bunge inayoshughulika na Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC), imemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Joseph Msambichaka, kutoa maelezo ya matumizi ya sh bilioni 20 zilizotumika katika mkutano wa wafanyakazi, matangazo na safari za ndani na nje za vigogo.
Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, alimtaka Msambichaka na Menejimenti ya TPA, kujipanga kutoa majibu sahihi ndani ya wiki mbili zijazo mjini Dodoma, watakapokuwa wanajadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2011/12 na 2012/13.
pichani niKaimu mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),Mzee Maden Kipande
Filikunjombe, alisema kamati yake haiwezi kujadili ripoti ya CAG kwa siku hiyo kwa kuwa waliipata juzi, hivyo hawajaisoma ili kupata hoja za kuzifanyia kazi.
Alisema alipopata ripoti ya TPA na kupitia kwa haraka haraka juzi, alibaini kuna matumizi mabaya ya fedha za walipakodi baada ya kubaini kuwa, mamlaka hiyo ilitumia sh bilioni 9.6 kwa ajili ya mkutano wa siku moja kwa wafanyakazi wake.
Alisema fedha zingine zilizotumika kwa matumizi mabaya ni sh bilioni 6.4 zilizotumika kwa ajili ya matangazo na sh bilioni 10 kwa ajili ya safari za nje na ndani kwa ajili ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
“Sasa Mwenyekiti wa bodi TPA, nawataka mkapitie vizuri ripoti hii ya CAG, baada ya wiki mbili mje na majibu sahihi….Mje mmeshiba chai kabisa,” alisema Filikunjombe.
Pichani ni WAZIRI wa Uchukuzi Dk Harison Mwakyembe 
Wakati huo huo, siku chache baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC) kumtuhumu aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe, kusababisha jiji hilo kupata hati chafu na kumtaka kwenda kujibu hoja, Mkurugenzi huyo amejitetea kuwa aliliacha jiji hilo likiwa na hati safi.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima huku akijibu maswali kwa ufupi, alisema alipoondoka katika Jiji hilo, aliliacha likiwa na hati safi na hiyo hati chafu imekuja baada ya kuondoka kwake.
Kuhusu kuhitajika kwenda kujibu tuhuma na hoja kutoka kwa kamati hiyo, Kabwe alisema hajapata taarifa za kuitwa na isitoshe kama Mkurugenzi hawajibiki kwa Kamati bali kwa mamlaka iliyomteua.
Kutokana na hilo, alisema endapo atapewa taarifa na wakubwa wake za kutakiwa kwenda Mwanza, atakwenda kwa sababu yeye ni mfanyakazi wa Serikali.
Wakihitimisha ziara yao katika Jiji la Mwanza, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Kangi Lugora, alisema ili kuwatendea haki Watanzania na wakazi wa Mwanza, kamati iliagiza kurudishwa kwa Mkurugenzi huyo kujibu hoja zilizojitokeza kwenye ripoti ya CAG.
Lugora, alisema cha kusikitisha ni kwamba pamoja na maagizo hayo, Wizara ya Tamisemi ambayo Wakurugenzi wapo chini yake, imeshindwa kufanya hivyo na kwa mazingira hayo inashindwa kuwatendea haki Watanzania ambao ndio walipa kodi wa fedha hizo zinazoliwa na wachache.
Juhudi za kumpata Naibu Waziri wa Tamisemi, Agrey Mwanri, kuzungumzia sakata hilo, ziligonga mwamba baada ya kupokea simu yake na kudai kuwa yupo kwenye kikao cha kamati za bunge.
Katika ripoti yake ya Hesabu za kufunga mwaka wa 2012/13 Ofisi ya CAG ilibainisha kuwa Halmashauri za Jiji la Mwanza, zinaongoza kwa kuwa na hati chafu.
Halmashauri zinazotajwa kuwa na hati zisizoridhishwa katika Jiji hilo ni pamoja na Halmashauri ya Sengerema, Magu, Misungwi na Mwanza.

Hakuna maoni