zitto achachamaa bungeni
Mjumbe wa Bunge la
Katiba, Zitto Kabwe amesema kuandikwa kwa Katiba isiyokubaliwa na pande zote
kutasababisha gharama kubwa kuliko zile zinazotajwa za serikali tatu.
Akichangia hoja
kwenye Bunge hilo jana, Zitto alisema kuna kila sababu ya kukaa na kukubaliana
ili kupata Katiba itakayokubalika pande zote.
"Muundo wa
Muungano una hatari ya kuvunjika iwapo hakuna matakwa ya dhati ya watu
kuungana... Maneno ya kusema Serikali tatu zitavunja Muungano ni ya siasa na
hayana msingi wa kisayansi. Urusi ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na
siyo sababu ya idadi ya Serikali," alisema.
Zitto ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema hofu ya
gharama inayotajwa katika uendeshaji wa muundo wa serikali tatu haina msingi
wowote kwa kuwa hakuna ushahidi wa kitaalamu unaothibitisha gharama hizo
.
"Nimesikia
watu wanasema eti tutalazimika kujenga ikulu mpya, nani kasema lazima tuwe na
marais watatu? Tunaweza kuwa na rais mmoja kwenye nchi na wakuu wa nchi
washirika wawili... Ni jambo la makubaliano tu," alisema.
Alisema bajeti ya
mwaka huu ni Sh18 trilioni, kati ya hizo Sh5.3 trilioni ndizo zinazohudumia
wizara za Muungano, lakini serikali ina uwezo wa kukusanya kodi zaidi ya Sh10
trilioni pamoja na mapato mengine.
"Kuna jumla
ya Sh2.3 trilioni hatuzikusanyi kila mwaka kutoka kwenye kampuni kubwa, kwa
uwezo wetu wa pato la ndani asilimia 17 tunao uwezo wa kuendesha serikali ya
muundo wa idadi yoyote.
"Hofu ya
Serikali ya Muungano kutokuwa na fedha ni sababu halisi, ni kweli kwamba ushuru
wa bidhaa pekee yake hauwezi kutuendeshea serikali. Sasa nini kazi yetu,
tunaingia hapa ili kuboresha hayo maeneo, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini
hapa?" alihoji.
Jussa akomaa
Mjumbe wa Bunge hilo,
Ismail Jussa jana alisisitiza kwamba Wazanzibari wengi hawapo tayari kuendelea
na mfumo wa serikali mbili kwa sababu unawatesa na kuwadhalilisha.
Jussa ambaye ni
mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia CUF, alisema haoni haya
kuzungumzia suala hilo kwa niaba ya Wazanzibari.
"Hoja nyingi
zimetoka (kuhusu Muungano), lakini naendelea kuzungumza kwa niaba ya wananchi
wa Zanzibar na katika hili sioni haya kwa sababu naamini kwamba wanakisimamia
kile ambacho sisi tunasimamia nacho ni Zanzibar yenye mamlaka kamili,"
alisema Jussa.
Alisema amekuwa
akijiuliza kwa nini serikali mbili zinang'ang'aniwa na CCM licha ya
kunung'unikiwa na baadhi ya wanachama wake kwa miaka 50?
"Hapa wala
maneno hayo hayajasemwa na CUF, wala na mpinzani. Hapa ninayo Ripoti ya Amina
Salum Ali ya Novemba 1992 ikiorodhesha matatizo lukuki ya mfumo wa serikali
mbili na wajumbe wake hawa wote walikuwa ni kutoka CCM, mwenyekiti wake Amina
Salum Ali, katibu wake Ali Juma Shamhuna ndiyo walioleta ripoti hii,"
alisema Jussa huku akionyesha ripoti hiyo.
Kutokana na hali
hiyo, alisema anaona ni kuwadanganya Wazanzibari kwamba serikali mbili
zitatatua matatizo yao, hivyo kuwafanya wajiulize mbona hazikuyatatua kwa miaka
50 iliyopita.(E.L)
Hakuna maoni
Chapisha Maoni