ZIARA YA RAIS MAGUFULI KENYA YABADILI HALI YA HEWA,SOMA HAPO KUJUA
RAIS John Magufuli leo amekutana na
Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya kwenye ziara yake ya kikazi na kubadili upepo wa
kisiasa uliokuwa unamwandama, anaandika Wolfram Mwalongo.
Akizungumza kwenye viwanja vya
Ikulu, Kenya Rais Magufuli amesema, anao uhusiano mzuri na Rais Kenyatta na
kwamba, waliokuwa wanadhani kuwa uhusiano huo una utata ‘hawakufikiri
sawasawa.’
“…Najisikia nipo nyumbani na bahati
nzuri Kenyatta namfahamu vizuri alipokuwa waziri wa tawala za mikoa…, huwa
tunapigiana simu na Uhuru Kenyata watu, wengi hawajui- mjue leo huwa
tunapigiana simu,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amekuwa akihusishwa na
siasa za upinzani nchini Kenya kutokana na uswahiba wake wa karibu na Raila
Odinga, aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo na aliyeingia kwenye mpambano na
Uhuru kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2012.
Kutokana na ukaribu wake, Rais
Magufuli akiwa waziri wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu aliwahi
kwenda Kenya na kuungana na Odinga kwenye kampeni zake jambo lililodhihiri
ukaribu wake.
Lakini pia, Aprili 2016 Odinga
alimtembelea Rais Magufuli Wilaya ya Chato, Tanzania wakati Magufuli
akiwa mapumziko.
Raila Odinga, aliyekuwa Waziri Mkuu
nchini Kenya akishuka kwenye Helkopta alipokwenda kumtembelea Rais John
Magufuli Chato, Tanzania.
Odinga alikwenda kusali na Rais
Magufuli katika kanisa la Bikira Maria Parokia ya Chato mkoani Geita kwenye ibada
ya jumapili ya pili ya Pasaka ambapo alipata nafasi ya kuwasalimia waumini wa
kanisa hilo.
“Nataka kuwathibitishia, ndugu yangu
Uhuru Kenyatta na Wakenya wote, ninyi ni ndugu zetu, mfano Kenya kuna Wamasai
pia Tanzania kuna wamasai, hata wanapotaka nyasi sidhani kama huwa wanaangalia
hata mipaka. Tanzania wapo Wajaluo, hapa wapo Wajaluo …..,” amesema.
Amesema kuwa, Kenya ndio mshirika wa
kwanza wa Tanzania katika uwekezaji na biashara barani Afrika na kwamba, hakuna
taifa jingine ambalo limewekeza nchini mwake kama Kenya.
Amesema kuwa, kulingana na rekodi za
uwekezaji nchini Tanzania kuna takriban kampuni 529 nchini humo kutoka Kenya
ambazo zinaingiza takriban dola bilioni 1.7 kila mwaka huku takriban Watanzania
57,260 wakiwa wameajiriwa.
Amewataka mawaziri wa mambo ya nje
wa pande zote mbili kukutana kabla ya mwaka kuisha ili kuona namana ya
kuboresha ushirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.
RaisUhuru amesema kwamba,
amefurahishwa na ziara ya Rais Magufuli nchini humo na kuwa, kufanya hivyo
kunadhihirisha umoja wao.
Amesema, ili mataifa hayo yapate
mendeleo ni lazima yafanye kazi kwa pamoja na kwamba, wamejadili namna ya
kuimarisha uchumi, ulinzi, mawasiliano na miundombinu ya Barabara ya Tanga
(Tanzania) mpaka Malindi nchini Kenya.
“Ili kupanua uchumi ni lazima Kenya
na Tanzania tutembee pamoja na mawazili wetu wa nje watakubaliana ili
kukamilisha hilo
“Tumeongea pia kuhusu usalama wa
nchi zetu pia tumekubaliana mambo ya mawasialiano, tupo na mpangao wa barabara
kutoka Tanga mpaka Malindi,” amesema Kenyatta.
Hii ni ziara ya tatu ya Rais
Magufuli tangu kuapishwa kwake Novemba mwaka jana ambapo alianza kutembelea
nchini Rwanda alipoenda kuzindua Daraja la Rusumo, ziara ya pili alikwenda
Uganda kwenye sherehe za kuapishwa Rais Yoweri Maseveni.