UVCCM KUMCHONGEA WAZIRI NDALICHAKO KWA MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Dakika
chache baada ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) taifa, kutoa
tangazo la kuwataka wanafunzi waliokosa mikopo wakati wana vigezo, kuandikisha
majina yao kupitia barua pepe ya UVCCM, jumuiya hiyo imeahidi kupeleka orodha
hiyo kwa Rais John Magufuli, anaandika Charles William.
Tangazo
la UVCCM limesema vielelezo vya kuthibitisha sifa za mwanafunzi kupata mkopo
ikiwemo vyeti vya kifo au vifo vya wazazi au hali ya familia anayotoka, vitumwe
kupitia barua pepe ya jumuiya hiyo ambayo ni uvccm1978@gmail.com huku mwisho wa kutuma
ni tarehe 4 Novemba 2016.
Akizungumza
na MwanaHALISI Online kwa njia ya
simu Sylvester Yaredi, Kaimu Katibu Idara ya Uhamasishaji, Sera, Utafiti na
Mawasiliano UVCCM, ametoa ufafanuzi wa tangazo hilo ambapo amesema watapeleka
orodha ya majina hayo kwa rais kwani wanaamini ataingilia kati suala hilo.
“Hatutachukua
fedha kutoka kwenye mfuko wa UVCCM ili kuwasomesha vijana waliokosa mikopo kama
baadhi wanavyodhani, tutachofanya ni kuandaa orodha ya wanafunzi pamoja na
vielelezo vinavyothibitisha sifa zao kupata mikopo.
Baada ya
hapo tutapeleka documents (nyaraka) hizo kwa Rais Magufuli kwasababu yeye
amekuwa akifuatilia suala hili kwa umakini, ndiyo maana amekuwa mkali mara kwa
mara kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu pale inapochelewesha malipo kwa
wanafunzi wa vyuo vikuu,” amesema Yaredi.
Kuipeleka
orodha hiyo kwa Rais Magufu huenda ikawa ni kumuweka kikaangoni Prof. Joyce
Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwani ndiye msimamizi wa
uwajibikaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu (HESLB).
Kwa kipindi
cha wiki tatu sasa tangu vyuo vikuu hapa nchini vilipoanza kufunguliwa, vilio
vya wanafunzi kukosa mikopo vimesikika vyuoni. Serikali imekuwa ikilaumiwa kwa
kupunguza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo.
Vigezo vipya
vya kupata mikopo vilivyotangazwa na serikali tarehe 12 Oktoba mwaka huu
kupitia kwa Mhandisi Stela Manyanya, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia ‘vimefinya’ wigo wa wanufaikaji. Hata hivyo, bado baadhi ya wale
wenye vigezo tajwa wamekosa mikopo hiyo.
Wiki mbili
zilizopita, Abdulrazaq Badru, Mkurugenzi wa HESLB aliwaeleza wanahabari kuwa
kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mkopo mwaka huu, watakaopewa ni 21,500 tu.
Siku nne baadaye Prof. Ndalichako alinukuliwa akisema, serikali itatoa mikopo
kwa wanafunzi 25,000.
Idadi hiyo
ni pungufu ya zaidi ya wanafunzi 15,000 ya waliopata mikopo mwaka jana ambapo
jumla ya wanafunzi 40,836 walipata mikopo.
Kama hilo
halitoshi, mchana wa leo Jumapili ya tarehe 30 Oktoba, 2016 Badru amewaeleza
tena wanahabari kuwa, HESLB itawapitia upya wanafunzi wanaoendelea na masomo
vyuoni ili kubaini ambao hawakidhi vigezo vipya na kuwaondoa.