UFISADI WA NSSF BALAA LAMWANGUKIA ZITTO KABWE,OLESENDEKA AFICHUA SIRI,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Serikali
kuhakiki akaunti na mali za Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT) na
wenzake waliokuwa katika kamati za fedha za Bunge, ili kubaini kama zinalingana
na kipato walichokuwa wakipata.
Msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka,
amesema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari, akimuhusisha Kiongozi
huyo Mkuu wa ACT na tuhuma za ufisadi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),
alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
”Nilikuwa najiuliza hivi chuki ya Zitto
kwa Serikali ya Awamu ya Tano, inayopambana na mafisadi imetoka wapi wakati
yeye alikuwa anasimamia mashirika hayo.
“Miongoni mwa taasisi hizo alizokuwa
akisimamia na baadhi ya marafiki zake ndiyo hao walionunua hekari moja kwa Sh
milioni 800, wakati ilikuwa ikiuzwa kwa Sh milioni 25 na walikuwa wamejificha
kwa maslahi binafsi,” alisema katika ofisi ndogo za Makao
Makuu, Lumumba Dar es Salaam.
NSSF ndiyo iliyonunua hekari 20,000 Kigamboni jijini
Dar es Salaam kwa Sh milioni 800 kwa kila hekari, badala ya Sh milioni 25 na
kujikuta katika hatari ya kupoteza Sh bilioni 270, katika mradi wa ujenzi wa
mji wa kisasa wa Dege Eco Village.
Kutokana na tuhuma hizo za NSSF zilizoibuka upya
katika kamati ya PAC wiki hii, Sendeka alisema ni vema Serikali ikague
kuona kama akaunti za viongozi wa zamani wa kamati hizo, maisha yao na mali
walizonazo, zinafanana na mapato halali waliyokuwa wakilipwa.
Alisema alikuwa anaangalia msukumo wa ghafla na
mapenzi ya akina Zitto waliyokuwa wanayapata kwa nchi, kumbe ilikuwa ni kichaka
cha kuficha baadhi ya maswahiba zao wasichukuliwe hatua.
Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Rais
Magufuli haina nia ya kurudi nyuma katika jambo lolote na kuwa itasonga mbele
huku akiamini kuwa Serikali iliyochaguliwa na watu haiwezi kufa.
“Tunahakika Serikali ya Magufuli iliyopata
ridhaa ya kutumikia watu, haitafutika kwa kelele za mlango wa baadhi ya
makuwadi na watu waliolipwa kuchafua taswira ya Tanzania,”
alisema.
Aliongeza kuwa Serikali hiyo itaendelea
kushughulikia wakwepa kodi pamoja na kuchunguza mambo aliyoanzisha
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa bandarini.
Kauli ya Zitto
Akizungumzia tuhuma hizo, Zitto Kabwe alisema hana
muda wa kujibu alichoita kuwa ni porojo na vioja vya Sendeka.
Alifafanua kuwa CCM ni chama dola na kuna taasisi
nyingi za uchunguzi za Serikali, ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) na Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP) na kushangaa kwa nini
vyombo hivyo havisemi, aseme Sendeka?