Zinazobamba

RAIS MAGUFULI ATOA MIKWARA MIZITO ,NI KWA WALE WASIOPENDA MUUNGANO,SOMA HAPO KUJUA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 26 April 2017, ameongoza maelfu ya Watanzania katika sherehe za miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukagua gwaride la vikosi vya ulinzi na Usalama lililoandaliwa kwa heshma yake, Rais Magufuli amewahakikishia watanzania kuwa yeye na Rais wa Zanzibara Dkt. Ali Mohamed Shein wataendelea kuulinda Muungano kwa nguvu zao zote na kwamba atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye.

''Muungano ndio silaha yetu. Ni nguvu yetu. Mimi na mwenzangu Dkt. Shein tutaulinda Muungano  kwa nguvu zote. Yeyote atakayejaribu kuuvunja atavunjika yeye'' amesema Rais Magufuli.

Aidha Dkt. Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini kwani amani ndio chachu ya maendeleo yanayopatikana nchini.

Rais Magufuli amesema Tanzania imeweza kufikisha miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa sababu ya amani iliyopo nchini iliyowezesha kupatikana mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuunganisha mataifa yetu mawili na kuuunda taifa moja lenye nguvu.

Aidha amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umewezesha kupatikana mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mhe. Rais ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na Muungano ni kukua kwa uchumi na kukabiliana na matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira,kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, majini,reli  na nchi kavu.

Aidha Muungano umeimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya shule na hospitali pamoja na kukua kwa demokrasia nchini.

Kwa mara ya kwanaza katika historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Maadhimisho ya Sherehe za Muungano zinafanyika mkoani Dodoma makao makuu ya Serikali ikiwa ni ishara tosha kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na chama cha Mapinduzi imedhamiria kwa dhati kuhakikisha makao makuuu ya Serikali yanakuwa Dodoma.

''Niwahahakikishie wana Dodoma na Watanzania kwa ujumla  kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi tena, na  kama tulivyoahidi mwaka 2020 Serikali yote itakuwa imehamia hapa'' amesema Rais magufuli.

Sherehe za miaka 53 ya Muungano zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajane wa viongozi waasisi wa Muungano mke wa hayati Mwalimu Julius Nyere Mama Maria Nyerere na hayati Abeid Aman Karume, Mama Shadya Karume,Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, na viongozi wa chama na serikali.

Kauli mbiu ya Sherehe za Muungano mwaka huu ni ''Miaka 53 ya muungano,Tuuulinde na kuuimarisha, Tupige vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii''

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
26 Aprili, 2017