Zinazobamba

'MUNGIKI WA PROF LIPUMBA';WALANIWA KILA KONA,MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA NA IDARA YA HABARI MAELEZO VYATOA TAMKO KALI,SOMA HAPO KUJUA


SIKU chache kupita baada ya watu wanaotajwa kutumwa na Mwenyekiti wa  Chama cha Wananchi (CUF) ambaye anatambuliwa na Ofisi ya Msaji wa Vyama vya Siasa nchini ,Profesa Ibrahimu Lipumba kuvamia mkutano wa Mwenyekiti wa Chama hicho wilaya ya Kinondoni na kupelekea kuwajuluhi waandishi wa habari na viongozi kadhaa wa CUF ambao wanaumuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho,Maalim Seif,

Hatimaye Sakata Hilo Limeibua Msajili wa vyama vya siasa nchini,Jaj Francis Mtungi na Kulaani tukio hilo huku akiwataka wanachama na viongozi wa Chama hicho wangojee hatma ya Mahakama ndio itakayomaliza mgogoro huo,

 TAMKO LA MSAJILI HILI HAPA 

Nimesoma na kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu vurugu zilizotokea tarehe 22 Aprili, 2017 katika hoteli ya Vina, Mabibo hapa Dar es salaam, zinazosemekana kuhusisha wanachama wa CUF.

Ni ukweli usiopingika kuwa, suala la mgogoro wa uongozi katika chama cha CUF lipo mahakamani, lakini nikiwa msimamizi wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kutambuliwa na jamii kuwa ni mlezi wa vyama vya siasa; nimelazimika kuwasihi wadau wa siasa hususani wanachama wa chama cha CUF, kutambua kwamba, kuwapo kwa shauri mahakamani siyo fursa ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani, kwani jambo hili ni uvunjifu wa sheria na linaleta sura mbaya kwa jamii.

Hivyo, ninalaani vurugu hizo, ambazo zilionekana kuvunja amani na utulivu na watu kuumizwa, tofauti na tunu zetu za taifa za amani na utulivu. Pia, nawaasa wanachama wa CUF pamoja na tofauti walizonazo, madhali masuala haya yapo mahakamani hebu tuheshimu utawala wa Sheria.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hata Jeshi la Polisi lipo kushughulikia malalamiko yoyote yanayohusu uendeshaji na shughuli za chama chochote cha siasa. Hivyo, hakuna haja ya wanachama wa chama cha CUF kukiuka taratibu za kuendesha chama hicho au kujichukulia Sheria mkononi.

Aidha, ninaviasa vyama vya siasa kuelewa kuwa havipo juu ya Sheria, vinapaswa kuheshimu na kufuata Sheria za nchi, ikiwamo kutunza amani na utulivu tulionao.

Mwisho, ninaomba vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi yetu kulifanyia kazi tukio hilo, ili wahusika wafahamike na kuchukuliwa hatua za kisheria. Kwa upande wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inayosimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria.

Jaji Francis S.K. Mutungi                            
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
24 Aprili, 2017
IDARA YA HABARI YATOA TAMKO KIPINGA HATUA YA KUVAMIWA WAANDISHI WA HABARI
Serikali imepokea kwa masikitiko taarifa za kushambuliwa na kujeruhiwa baadhi ya waandishi wa habari katika mvutano uliotokea juzi jijini Dar es Salaam kati ya wafuasi wa pande mbili zinazokinzana za Chama cha Wananchi (CUF). Tumechukua muda kidogo kulifuatilia suala hili na kubaini licha ya baadhi yao kujeruhiwa na kuripoti polisi, wapo waandishi ambao vifaa vyao vya kazi pia vililengwa katika shambulizi hilo.

Tunachukua fursa hii kulaani kitendo cha kuumizwa wanahabari tena waliokuwa wamealikwa kuhudhuria mkutano huo. Ifahamike kuwa uandishi wa habari ni taaluma adhimu na nadhifu inayopaswa kuheshimiwa, kuenziwa, kulindwa na kutoingizwa katika migogoro ya pande zinazofarakana katika jamii.

Kifungu cha 7 (1) (a) cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 kinaainisha uhuru wa wanahabari katika kukusanya habari kwa muktadha wa kuwepo katika maeneo ya matukio kama hakuna sababu nyingine za kuzuiwa. Misingi ya uhuru huu wa kitaaluma pia imesisitizwa katika Ibara za 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 ambao nchi yetu imeuridhia.

Tunawatakia nafuu ya haraka wanahabari waliojeruhiwa na wenzao wengine waliopatwa na jakamoyo katika tukio hilo. Kwa kuwa suala hili tayari limeripotiwa polisi, tunawaomba wadau wote wa habari na wanasiasa kwa sasa kutulia na kuviachia vyombo husika vilifanyie kazi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe.

Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali