WAZIRI NAPE NA SERIKALI YAKE WAANGUKIA "PUA" MAHAKAMANI,KESI YA GAZETI LA MAWIO,SASA KUREJEA MTAANI,SOMAHAPO
HATIMAYE gazeti la MAWIO lililofutwa na serikali ya Tanzania na kuacha
kuchapishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja, limerejea mtaani kwa uamuzi wa
Mahakama Kuu.
Serikali ililifuta gazeti hilo na kulizuia kuchapishwa kwa njia yoyote ile Januari 15, mwaka jana- 2016.
Uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa Jumanne ya wiki hii, umetupilia mbali
amri ya serikali ya “kuliua na kulizika kabisa” gazeti hilo lililokuwa
likitoka kila wiki – Siku ya Alhamisi.
Mahakaka Kuu ilisema kuwa amri ya serikali kuliua MAWIO haikuwa sahihi, hivyo “gazeti hilo lilionewa.”
Jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Sakieti Kihiyo, limesema
gazeti la MAWIO halikupewa nafasi ya kujitetea kabla ya hatua ya
serikali ya kulifuta kutoka orodha ya msajili wa magazeti nchini.
Msajili wa magazeti nchini ni Idara ya Habari Tanzania (MAELEZO).
Jaji Ignas Kitusi ndiye alisoma uamuzi wa Mahakama kuu – kwa niaba ya
jopo siku ya Jumanne, wiki iliyopita (Februari 28). Jaji mwingine
aliyekuwa kwenye jopo hilo, ni Jaji Ama-Isario Munisi.
Serikali ililifuta gazeti la MAWIO tarehe 15 Januari 2016 baada ya kudaiwa kuandika ilichoita habari na makala za “kichochezi.”
Utawala wa Kampuni ya Victoria Media Services Limited, wachapishaji wa
gazeti la MAWIO, uliamua kufungua kesi mahakamani. Hii ni kesi Na. 15 ya
mwaka 2016.
Wakili wa MAWIO, Dk. Rugemeleza Nshalla, ameiambia FikraPevu kuwa hatua ya serikali iliegemea falsafa ya “…Nyonga kwanza na sikiliza baadaye.”
Dk. Nshalla amesema katika mazingira yoyote yale, sharti walalamikiwa
wapate nafasi ya kujieleza na kusiklilizwa na mahakama kwanza kabla ya
hukumu kutolewa.
FikraPevu
lilimpata Mkurugenzi Mtendaji na Mhariri Mkuu wa gazeti la MAWIO, Simon
Mkina ambaye amesema alishangazwa sana na hatua ya serikali kufuta
alichoita “mdomo wa wananchi.”
“Kufuta chombo hiki au kingine kama hiki, ni kukiri kuwa serikali
haipendi kusikia kutoka kwa wananchi…” amesema Mkina katika mahojiano na
FikraPevu.
Mkina amesema MAWIO limekuwa gazeti linalozingatia maadili na kufuata
weledi wa hali ya juu katika kuandika na kuchapisha habari na makala na
kuongeza kuwa limekuwa gazeti pekee linalotoa uwanja mpana kwa wananchi
kuandika mawazo yao ili kuchochea uwajibikaji wa viongozi wa serikali.
Mkina amesema kufuatia uamuzi huo wa Mahakama Kuu, MAWIO litarejea
mtaani Alhamisi ya wiki hii na kuahidi kuwapa wasomaji wake habari
zilizofanyiwa kazi ya ziada.
“Kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja, wakati gazeti halipo mtaani – likiwa
limefutwa na serikali, pamoja na kupoteza ajira za watu na kuingia
katika hasara kubwa, bado tulikuwa na kazi ya kujiuliza ni wapi
tulikosea na je, lini tutapewa haki yetu? Bahati nzuri haki yetu
imefika,” aliongeza Mkina akiongea na FikraPevu.
Uamuzi na hatua ya kulifuta MAWIO, lililokuwa likichapishwa kila Alhamisi, ulitangazwa na Nape Nnauye, Waziri wa habari, vijana, utamaduni, sanaa na michezo.
Tangazo lililotolewa katika gazeti la serikali, Na. 55 la Januari 15,
2016, lilisema serikali inachukua uamuzi wa kulifuta kwa mujibu wa
mamlaka iliyonayo kupitia Sheria ya Magazeti ya 1976; sura ya 229
kifungu cha 25(1).