Zinazobamba

WAUZA ‘UNGA’ WAJA NA MBINU MPYA






Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
VITA bado mbichi. Ndivyo unavyoweza kusema, hasa baada ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini kubuni njia mpya ya kuwaangamiza vijana wanaotumia mihadarati hiyo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Serikali kutangaza mapambano dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara na utumiaji wa dawa za kulevya, chini ya oparesheni iliyoasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Baadhi yawafanyabiashara maarufu pamoja na kundi la wasanii jijini Dar es Salaam walitajwa kuhusika na biashara hiyo huku baadhi yao wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma dhidi yao.
MTANZANIA ilifanya uchunguzi wa kina wa takribani wiki moja baada ya oparesheni hiyo na kubaini kuwa wauzaji wa bishara hiyo haramu sasa wameamua kubadili mbinu na kuamua kuwatumia wang’arisha viatu pamoja na baadhi ya vibanda vya mawakala wa fedha wanaotoa huduma za fedha kwa njia ya simu.
Mbinu hiyo ni dhahiri imeonekana kama njia mbadala baada ya baadhi ya watumiaji wake ‘mateja’ kulalamika katika siku za hivi karibuni kuwa wapo hatarini kupoteza maisha kutokana na kukosa dawa hizo ambazo zimekuwa zikiwaangamiza zaidi na hata kuonekana kama wendawazimu.
‘Mateja’ wengi ambao walikuwa wakionekana maeneo ya wazi kama vile kwenye maeneo ya michezo ya kamari,  vituo vya daladala hivi sasa wamepotea kwa kuhofia kukamatwa na hata wengine wakionena katika meza za wangarisha viatu ambao uhusiasha katika uuzaji wa biashara hiyo.
Maeneo ambayo gazeti hili limebaini hutumiwa  na wafanyabiashara hao ni Kinondoni Manyanya, Mkwajuni, Yombo Makangarawe kituo cha daladala, Majimatitu Stendi, Mbagala Rangi Tatu, Posta Mpya na zamani , Yombo Lumo, Mbagala Kibonde Maji.
Mwandishi wa gazeti hili aliweka kambi kwa siku nne mfululizo katika kituo cha daladala Kinondoni Manyanya ambapo mmoja wa wamiliki wa maduka katika eneo hilo, alieleza mbinu zinazotumika sasa huku MTANZANIA ikishuhudia wang’arisha viatu namna wanavyosambaza dawa hizo kwa njia ya siri.
“Hebu angalie pale mbele kwa yule ‘Shoe shine’ mng’arisha viatu unamwona anampa kitu yule mtu ‘teja’ kwa kificho ule ni unga ‘dawa za kulevya’. Tena yule huletewa kila siku pale na mtu ambaye huja na pikipiki na hupita tena kila inapofika saa 11:30 jioni.
“Huu ni utaratibu unaweza kusema ni mpya lakini si mpya kwani mtindo huu umekuwa ukitumiwa muda mrefu sana na hasa tangu ilipoonekana hakuna udhibiti wa kina wa bishara ya dawa katika eneo letu.
“Tena unamwona mtu anajenga na hata wakati mwingine ana gari zuri eti kwa kazi ya kung’arisha viatu kumbe hapa kuna kazi nyingine kama hiyo unayoiona ‘dawa za kulevya’,” alisema mfanyabishara huyo ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama.
Katika eneo la Kinondoni Mkwajuni gazeti hili lilishuhudia kundi la vijana kituoni hapo wakienda katika moja ya kibanda cha huduma za fedha kwa njia ya mtandao wakitoa fedha na kupewa ‘unga’ kwa kificho.
Vijana hao walikuwa wakienda katika kibanda hicho moja mmoja huku wakiwa makini kuangalia hali ya usalama wao na kisha baada ya kununua huvuka barabara na kelekea eneo la Kinondoni Moscow ambapo huenda kuvuta dawa hizo kwa njia mbalimbali ikiwemo kujidunga kwa sindano.
“Dada vipi mbona unaonekana upo hapa muda mrefu una shida gani sema shida yako tukusaidie maana hatukuelewi,” alihoji mmoja wa vijana wenye vibanda ambavyo vinasadikiwa kufanya bishara katika eneo hilo.
Baada ya maelezo hayo mwandishi alimjibu kwa kifupi kijana huyo kuwa alikuwa akimsubiri mtu ambaye aliahidiana wakutane hapo kwa lengo la kwenda katika moja ya ofisi ambayo mwenyeji wake alikuwa akiifahamu ilipo.
Mbali na uwepo wa hofu ya kukamatwa baadhi ya maduka wamelazimika kuweka matangazo maalumu kwenye milango yao wakionya watu kutosimama nje ya maduka yao kama si wateja.
Matangazo hayo yalisomeka “Tangazo, Tangazo, Tangazo, Ni marufuku mtu yeyote kukaa mahali hapa bila shughuli  yoyote, vinginevyo  uwe mteja unayetaka huduma katika eneo hili, hatua kali zitachukuliwa ikiwa umeonekana hapa kama huna kazi au si mteja,” yalisomeka matangazo hayo yaliyobandikwa kwenye milango ya maduka.
Wakati mwandishi wakiwa amepiga kambi katika eneo hilo jirani na Msikiti wa Mkwajuni, mmoja wa wanafunzi wa kiume alionekana amevaa sare za shule ya msingi ambaye hutumika kwa ajili ya usambazaji wa dawa za kulevya alikuwa akifanyakazi hiyo katika baadhi ya vibanda.
“Huyu mwanafunzi unamwona hapo ndiyo wanamtumia angalia baada ya muda utamwona anakuja tena na anatoa au kupokea kitu, hivyo watoto wetu wanaharibika vizazi baada ya vizazi tunaomba hii vita ifanikiwe kwa kweli,’’alisema mfanyabiashara mmoja hakutaka jina kutajwa gazetini.
Katika eneo la Posta Mpya wasambazaji hao wa dawa za kulevya wamekuwa wakitumia mbinu ya kuwatumia wauzz vocha na wang’arisha viatu waliopo katika kituo hicho.
WENYEVITI WA MITAA WALONGA
Wakizungumza na MTANZANIA Mwenyekiti wa Serikali Mtaa wa Mtambani Vingunguti, Mohamed Mtutuma alisema katika kituo cha daladala vijana wengi wamekimbia .
Alisema waliposikia tangazo la kuwataka kujisalimisha walihama kijiwe hiko na kwa sasa kuko kweupe hata msongamano umepungua.
Alisema kuhusu kuwatumia wafanyabiashara waliopo kwenye kituo hiko, hajagundua hilo labda aanze kuchunguza na kama lipo ataripoti.
Mwenyekiti wa Serikali Mitaa Kibonde Maji,  Juma Kanali alisema tatizo hilo katika mtaa wake lilikuwepo lakini si ‘unga’ bali ni bangi.
Mwenyekiti wa Maji Matitu Stendi, Said Mpeta alisema baada ya tangazo la kuwataja na wengine kuwataka kujipeleka wenyewe  hali imekuwa nzuri kwa upande wao.
“Kwetu tupo vizuri kidogo maana ilikuwa sana kuvuta bangi na si unga lakini tangu waanze kutajana watu wamekimbia na mimi nikiletewa jina nalichunguza na kulipeleka bila kusita maana lengo ni kupambana na dawa za kulevya ,’’
Kwa upande wake Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka hiyo, Mihayo Msikhela, alisema hiyo ni vita na hao ni binadamu hivyo nao wamekuwa wakibuni njia mbalimbali za kuhakikisha wanafanikiwa wanachokitaka.
“Vita zina mbinu nyingi na binadamu anabadilika kutokana na mazingira aliyopo hivyo inabidi tuwe tunashirikiana katika hili,” alisema Kamishna Msikhela
Alisema atahakikisha wanatoa maelekezo kwa timu yao ili wajiingize katika kila maeneo kwa kwa kushtukiza na kuwabaini kama kwenye meza za biashara hao kama kuna viashiria vya biashara ya dawa za kulevya.