WANAHABARI WALAUMIWA KWA KUCHANGIA UMASIKINI TANZANIA.HAPO KUJUA
I
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba (kulia), akizungumza na wanahabari Dar es Salaam leo, wakati akimkaribisha Mwanachama wa Kituo hicho, Ananilea Nkya (katikati) kuzungumzia utafiti wake alioufanya kuhusu namna vyombo vya habari vya Tanzania vinavyojishughulisha na maendeleo. Kushoto ni .Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga.
Mwanachama
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ananilea Nkya
(katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi Dar es Salaam leo,
juu ya utafiti alioufanya kuhusu namna vyombo vya habari Tanzania
vinavyojishughulisha na maendeleo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC,
Dk.Helen Kijo-Bisimba na .Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga
Taarifa ya utafiti huo ikiendelea kutolewa.
Mwanahabari Hilda wa gazeti la Daily News akiwa mzigoni.
Maofisa wa LHRC wakifuatilia mkutano huo
UTAFITI uliofanywa na Mwanachama wa Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu (LHRC), Ananilea Nkya, kama sehemu ya masomo yake ya
Shahada ya Uzamivu (PhD), umebaini kuwa habari zinazotangazwa
na vyombo vya habari hapa nchini hazichangii ipasavyo juhudi za taifa
katika kutokomeza umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi ambao
wanaishi vijijini.
Utafiti huu umabainisha kuwa sababu kubwa ni kwamba
habari zinazotangazwa na vyombo vya habari zinajikita zaidi katika
matukio yanayotokea mijini, na wanaopatiwa fursa kubwa ya kutoa
maoni ni wanaume ambao ni watumishi wa umma na wanasiasa.
Utafiti huu umehusisha habari 10,371
zilizotangazwa katika vyombo vya habari 15 katika muda wa mwezi
mzima Febuari 2014.
Habari hizo zilitangazwa kwenye taarifa ya habari ya
saa mbili usiku kwenye televisheni mbili na radio mbili za
kitaifa na zilizochapishwa katika magazeti 11 ya
kila siku. Utafiti ulilenga kupata majibu ya swali: Vyombo vya
habari Tanzania vinaripoti masula gani ya maendeleo na kwa mtazamo
wa watu gani? Kati ya habari 10,371 zilizofanyiwa
utafiti 9,607 zilichapishwa magazetini.
Utafiti huu unaonesha kuwa kati ya habari 10,371
zilizochapishwa 4,750 (45.8%) zilitokea Dar es Salaam na 5,621 (54.2%)
zilitoka mikoani na Zanzibar.
Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa kkoa wa Dar
es Salaam ulinufaika zaidi kimaendeleo kwa sababu kama habari hizo
10,371 zingegawanywa kwa usawa kwa mikoa yote, kila
mkoa ungepata fursa ya kutoa habari 368 kuhusu mambo mbali mbali yanayohusu
maendeleo ya wananchi wake.
Habari hizo zingekuwa ni fursa ya mikoa kutangaza,
ili kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha wananchi kujadili changamoto
na mafanikio ya maendeleo yao katika nyanja ya kijamii, kiuchumi na
kisiasa
Kwa kufanya hivyo wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja
na wanachi wenyewe, serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, mashirika ya
kijamii (NGOs), taasisi za dini, taasisi za elimu, taasisi za fedha na
wafadhili wa nje wanaochangia maendeleo ya nchi yetu wangechukua hatua
sahihi na kwa wakati husika kushughulikia matatizo yanayosababisha
wananchi wengi kuishi maisha ya kimaskini.
Hata hivyo badala ya vyombo vya habari vya
kitaifa kuwa chachu ya maendeleo kwa kutangaza habari zinazoweza
kuinua maendeleo kila mkoa, kila wilaya na kila kijiji, habari
nyingi tena za kimatukio tu zisizofanyiwa uchunguzi zinaufanya mkoa wa
Dar es Salaam kuchukua fursa 15 za maendeleo kupitia habari
ambazo kila mkoa hapa nchini ungepata kila mwezi kujadili
masuala ya maendeleo yanayohusu watu wake.
Masuala ya maendeleo yayosumbua wananchi
wengi katika mikoa mingi hapa nchini ni pamoja na ukosefu wa
ajira/kipato, ukosefu wa maji safi na salama, elimu bora, huduma bora ya afya,
ukosefu wa umeme na barabara.
Aidha utafiti huu umebaini kuwa habari
zinazotangazwa na vyombo vya habari vya kitaifa ziko zaidi katika
mtazamo wa watumishi wa umma kwa sababu ndio wanaonukuliwa
zaidi kwenye habari hizo.
Kati ya watu 14,637 walionukuliwa kwenye habari
10,371 zilizohusishwa kwenye utafiti, watu 8,398 (57.4%) walionukuliwa
walikuwa ni watumishi wa umma, 1,945 (13.3%) ni wanasiasa
2,757 (18.8%) wawakilishi wa taasisi za kiraia na mashirika binafsi (CSOs) na
wananchi wa kawaida walionukuliwa walikuwa 1,199 (10.5%).
Hata hivyo kwa vile kuzungumza kwenye vyombo
vya habari ni fursa inayoweza kudidimiza au kuharakisha maendeleo, fursa
hizo 14,637 zingegawanywa sawa kwa makundi yote--- wananchi,
watumishi wa umma, wanasiasa, taasisi za kiraia na mashirika
binafsi, kila kundi lingepata fursa 3,659 kuzungumza kupitia vyombo
vya habari kuhusu masuala ya maendeleo.
Hivyo kwa mujibu wa utafiti huu maafisa wa umma
walipata fursa mara tano zaidi kuliko wananchi wa kawaida
kuzungunza kupitia habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya
kitaifa.
Aidha walipata fursa mara nne zaidi
kuliko wanasiasa na mara tatu kuliko wawakilishi wa taasisi za kiraia na
mashirika binafsi.
Katika utafiti huu maafisa wa umma ni
viongozi na watumishi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi taifa,
mashirika ya umma, mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye ofisi zake hapa nchini
na maafisa katika balozi zenye ofisi zake Tanzania.
Wanasiasa ni wawakilishi kutoka vyama
vya siasa. Taasisi za kiraia na mashirika binafsi inajumuisha
vyama vya kitaaluma, vyama vya wafanyakazi, taasiasi za dini,
mashirika binafsi, shule na vyuo binafsi na kundi la wananchi
linajumuisha wanachi wa kawaida wanaume na wanawake.
Kadhalika utafiti unaonyesha kuwa habari zilizochapishwa
na magazeti, kila habari kwa wastani ilinukuu mtu (chanzo cha
habari) mmoja wakati kwa redio na televisheni, kwa wastani, kila
habari ilinukuu si chini ya watu wawili.
Utafiti huo unaonyesha kuwa habari
zinazotanganwa na vyombo vya habari vya kitaifa zinajihusisha zaidi
na maendeleo ya wanasiasa kwa sababu habari zinazonukuu
wanasiasa ndizo zinapewa umuhimu mkubwa zaidi katika vyombo vya
habari.
Kati ya habari 411 zilizotangazwa
kama habari Kuu (lead stories) katika vyombo hivyo 15 habari
234 (57%) zilikuwa za kisiasa, 121 (29%) zilijadili masuala
ya kijamii na 56 (14%) uchumi. Hii ina maana kuwa vyombo vya habari
haviyapi umuhimu masuala ya uchumi ambayo ndiyo yanafanya
wananchi wengi kuwa maskini.
Kwa mfano utafiti unaonyesha kuwa kati ya
habari kuu 411, habari 307 (74.7%) zilichapishwa kwenye magazeti
magazetini 11 kama habari kuu. Hata hivyo kati ya habari hizo 307,
habari zilizojadili masuala ya kijami mfano shule afya na umeme zilikuwa 67
(22%), uchumi ni 39 (12.5%) na 201 (65.5%) zilikuwa ni siasa.
Habari za siasa ziliandikwa kutokana na
mikutano ya kisiasa, mahojiano na wanasiasa, kampeni za uchaguzi, taarifa
za vyama vya siasa kwenye vyombo vya habari, makongamamo na washa za kisiasa.
Habari za uchumi ni zile zilizohusu masuala ya
rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi,
ukusanyaji kodi kupitia mashine za kieletroniki (EFD), kilimo, matatizo ya
wakulima katika kupata pembejeo na masoko ya mazao yao, uchimbaji madini,
utalii, viwanda, uwekezaji, matatizo ya ajira, mabadilisho ya fedha, biashara
na ujasiriamali, uvuvi na misitu ikiwepo ukataji miti kupata magogo
kwa ajili ya biashara ya mbao.
Habari za kijamii ni zile zilizojikita kwenye
haki za binadamu, jinsia, mimba mashuleni, kuozesha kwa nguvu watoto wa
kike, ukatili majumbani, biashara ya binadamu na migogoro ya ardhi.
Zilihusisha pia masuala ya elimu kama vile
uhaba wa walimu, vitabu na madawati katika shule za umma
(serikali), uhaba wa chakula, ajali za barabarani, miundo mbinu, masula ya
kisheria, masuala ya dini, na habari za mahakamani.
Vyombo vya habari vya umma vya utangazaji
vilivyohusishwa kwenye utafiti huu ni TBC 1 na TBC Taifa wakati vyombo
vya habari vya watu binafsi ni pamoja na ITV na Radio One. Magazeti ya kila
siku ya Kiswahili yalikuwa ni Nipashe, Mwananchi, Mtanzania, Majira, JamboLeo
and Tanzania Daima. Na magazeti ya Kiingereza yalikuwa the Citizen na the
Guardian na gazeti la serikali Daily News.
Utafiti unaonyesha pia kwamba habari
zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Tanzania zilitawaliwa na mfumo
dume ambapo kati ya watu 14,655 walionukuliwa katika taarifa 10,371 kwenye
vyombo vya habari 15, wanawake walikuwa 2,646 (18%) na wanaume 12,009
(82%).
Utafiti unadhihirisha jinsi ambavyo maoni yanayohusu
maendeleo yanayowasilishwa kupitia habari yanavyotawaliwa na wanaume.
Watu 14,637 walionukuliwa kwenye taarifa za habari
walinufaika na nafasi ya vyombo vya habari kama fursa ya maendeleo kwa sababu
waliweza kuwasilisha maono yao ambayo yalichagiza mipango ya maendeleo ya taifa
.
Hii inadhihirisha kwamba hoja/maoni
yaliyotolewa na watu hao 14, 637 yangehesabiwa kuwa fursa za
maendeleo na kugawanywa kwa uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume kama
makundi ya kijamii kila kundi lingepata fursa 7,318 ya kuzungumzia
masuala ya maendeleo kwa mtazamo wao.
Hivyo basi kwa dhana kwamba idadi ya wanaume
walionukuliwa katika taarifa za habari ni 82% na wanawake ni 18%, inamaanisha
kwamba wanaume walikuwa na nafasi mara tano Zaidi ya wanawake katika kupata
fursa kwenye vyombo vya habari kama sehemu ya kuwasilisha maoni yao ambayo
yalichechemua mipango ya taifa ya maendeleo.
Hii inaonyesha jinsi ambavyo wanawake ambao ndio
sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini Tanzania wanakosa fursa. Utafiti huu
umeonye wanawake wanakosa fursa mara tano ikilinganishwa na wanaum,e katika
kuzungumza kwenye vyombo vya habari .
Utafiti huu unaonyesha kuwa masuala ya
kimaendeleo yanayowagusa wanawake kama kundi kubwa katika jamii linalojumuisha
zaidi ya 51% ya idadi ya watu nchini yameendelea kutokushughulikiwa. Kwa
mfano , kutokana na hali hiyo wanawake walio katika umri wa kuzaa wameendelea
kuhatarisha maisha kwa vifo ambavyo vingeweza kuzuilika wakati wa
kujifungua.
Sambamba na hilo wanawake wengi wameendelea kutumia
muda mwingi kutembea umbali mrefu wakitafuta maji na kuni kwa sababu ya
kutokuwepo kwa mabomba ya maji na umeme. Na hivyo kudumaza uchumi wa faimilia
zao na taifa.
Kwa upande wa magazeti kati ya watu 12,822
walionukuliwa 2371 (18.5%) walikuwa wanawake na 10,451 (81.5) walikuwa
wanaume.
Hii inamaana kuwa taarifa za habari zilizochapishwa kwenye magazeti 11 ya kila siku, kwa wastani wanaume walikuwa na fursa mara nne zaidi kulinganisha na wanawake kutoa maoni yao juu ya masuala ya maendeleo.
Hata hivyo, gazeti la Daily News lilikuwa na 24% ya
wanawake ambao maoni yao juu ya maendeleo yalipenyeza kwenye uwanda wa habari.
Hii inamaanisha kwamba kupitia taarifa za habari za Daily News. Wanaume
walikuwa na nafasi mara tatu Zaidi ya kujadili masuala ya kimaendeleo kuliko
wanawake.
Katika upande mwingine, gazeti la Mtanzania na the
Citizen uwakilishi wa wanawake ilikua 16%, na 16.2% kwa kila moja ambapo hii
inaonyesha ni jinsi gani magazeti haya mawili yalimpa mwanaume nafasi mara tano
Zaidi ya mwakamke katika kujipambanua katika masuala ya kimaendeleo.
Kadhalika utafiti unaonyesha kuwa habari
zinaandikwa zaidi na wanaume . Utafiti unaonyesha kwamba wanahabari 8,094
walihusika katika ukusanyaji wa taarifa zilizotumika kuunda taarifa za habari
10,371 ambazo zilitolewa kwenye vyombo vya habari 15 vilivyofanyiwa utafiti
katika utafiti huu. Miongoni mwa walioandika bahari hizo, wanahabari
3,039 (37.6%) walikuwa wanawake na 5,053 (62.4%) walikuwa wanaume.
Hii inaonyesha jinsi ambavyo waandishi wa kiume
wanapata fursa karibu mara mbili ikilinganishwa na wanahabari wa kike
katika kuandaa habari juu ya masuala ya maendeleo. Hii inatoa maana
kwamba waandishi wanawake wamepoteza fursa kuandaa habari zinazohusu maendeleo
ya nchi kwa mtazamo wa wanawake ambazo zingeweza kuibua masuala
yanayoathiri wanawake katika maendeleo na kuweza kushughulikiwa.