TUNAMUOMBA RAIS ATUMIE MAMLAKA YAKE KUTANGAZA BALAA LA NJAA TANZANIA: ACT-WAZALENDO
Chama Cha ACT –Wazalendo kimesema tatizo la njaa
bado lipo Nchini na kwamba kama Taifa hatua za makusudi zinapaswa kuchukuliwa ikiwemo
kutangaza balaa hilo ili kuwaokoa wananchi wa hali ya chini.
Hayo yamebainishwa na katibu wa kamati ya maendeleo
ya jamii kutoka chama cha ACT-Wazalendo Bi. Janeth Rithe wakati akizungumza na Waandishi
wa habari ofisini kwake.
Amesema kwa mujibu wa utafiti walioufanya kupitia
mikoa minane, wamebaini kuwa chakula muhimu kama unga wa mahindi na Maharagwe
zimeanza kuadimika na kusababisha bidhaa hiyo kuongezeka bei kwa kasi
ukilinganisha na miezi mitatu ya Nyuma.
“Takwimu zetu zinaonyesha kuwa bei ya unga, maharage
na vyakula vingine muhimu kwa wananchi walio wengi vimepanda kutoka shilingi
900/= kwa kilo katika miezi mitatu iliyopita hadi kufikia shilingi 2000/= kwa
hivi sasa” Alisema
Amesema kupanda kwa bei ya vyakula hivyo muhimu kwa
kasi kubwa namna hiyo ni kiashiria tosha kuwa upatikanaji wa vyakula hivyo
umeshuka sokoni na hivyo kufanya mahitaji kuwa makubwa kuliko usambazaji wake.(supply
and demand concept)
Amesema utafiti
huo unaonyesha kuwa Mkoa wa Arusha bei ya unga wa mahindi kwa sasa ni Shilingi
1700, wakati bei ya Maharagwe ni Shilingi 2200, Jiji la Dar es Salaam Bei ya
unga wa mahindi ni Shilingi 2000, huku bei ya Maharage Shilingi 3000, Mkoa wa
Dodoma bei ya mahindi 1600 na maharage
Shilingi 2200 na Mkoa wa Morogoro bei ya unga wa mahindi 18,000 na
maharage 18,000.
“Kutokana na hali ya chakula nchini, na hali ya
maisha kwa wananchi kwa ujumla, Chama cha ACT Wazalendo kinatoa wito kwa
serikali ya CCM kuchukua hatua za haraka kurekebisha mambo, ikiwemo kuchochea
Tija kwenye Kilimo.” Alisema
Ameongeza kusema uamuzi wa Serikali ya CCM kupunguza
bajeti ya ruzuku ya mbolea kutoka shilingi bilioni 78 mwaka 2015/16 mpaka
bilioni 10 mwaka 2016/17 haukuwa uamuzi sahihi na umechangia katika
kuwapunguzia wananchi uwezo wa kuzalisha.
Serikali inapaswa kuchochea kilimo kwa kuongeza bajeti
eneo hilo ili kukuza uzalishaji ambao umeanza kushuka kutoka 2.5% kwaka 2016
hadi kufikia 0.6% kwa sasa.
Tunataka Serikali itenge pesa kwa ajili ya kilimo
cha umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa kilimo cha mvua ambazo zinazidi
kutokutabirika. Serikali ijenge maghala
ya kutosha na Bunge liongeze bajeti ya hifadhi ya Chakula ya Taifa. Alisema
Kutokana na hali ya ukame katika mikoa mingi nchini,
na hali ya chakula kuendelea kudorora, tunamshauri Rais atumie mamlaka yake
kikatiba kutangaza rasmi janga la ukame nchini na hali mbaya ya chakula.